Na Josea Sinkala, Mbeya.
Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Mbeya, limepitisha bajeti ya zaidi ya shilingi billion 60 kwa ajili ya kutumika na Halmashauri ya wilaya ya Mbeya katika miradi na nmipango mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Mbeya.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa ajili ya kutumika kwa kipindi cha mwaka 2025/2026, mkuu wa idara ya mipango na uratibu katika Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Bi. Francisca Nzota, amesema jumla ya bajeti kuu shilingi billion 66.6 zimepangwa kukusanywa kupitia vyanzo mbalimbali ambapo kati yake kuna mishahara kwa watumishi kwa asilimia kubwa na fedha za miradi shilingi billion 12 ili kutoa huduma bora kwa jamii katika sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu.
Wakichangia maoni kwenye kikao hicho cha bajeti, madiwani wameonyesha kuunga mkono mapendekezo ya bajeti hiyo kwa kugusa baadhi ya maeneo muhimu na zaidi kugusa kata zote 28 za Mbeya vijijini.
Pamoja na hayo madiwani hayo wameishauri Serikali kuongeza vyanzo vya mapato ili kuongeza wigo wa mapato ya Halmashauri kwa ajili ya kurejesha kupitia shughuli za maendeleo kwa maslahi ya jamii yenyewe ikiwemo kwenye eneo la mazao hasa viazi mviringo, kwenye madini na ujenzi miradi mbalimbali ya kuiingizia mapato Halmashauri.
Baraza limepokea mapendekezo ya madiwani na kujibu baadhi ya hoja ili kuboresha zaidi eneo la upatikanaji zaidi wa mapato ya Halmashauri ambapo madiwani wa Halmashauri ya Mbeya kwa pamoja baada ya kupokea na kuipitisha bajeti hiyo wamekubaliana kuwapongeza wataalam (watumishi) wa Halmashauri kwa kuwapa motisha kutokana na ushirikiano wao katika kuleta ufanisi wa kazi katika maeneo yao.