Latest Posts

BAWACHA NYASA WAIJIA JUU G55 YA CHADEMA

 

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Baraza la wanawake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA (BAWACHA) Kanda ya Nyasa, limekemea vikali kuibuka kwa kundi linalojulikana kwa jina la G55 linalopinga kampeni ya No reforms no election.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya mnamo Aprili 08, 2025, mwenyekiti wa BAWACHA kanda ya Nyasa Tabia Kilasi Mwakikuti ameeleza kusikitishwa kwake na kuwepo kwa baadhi ya wana CHADEMA wanaopinga kampeni ya no reforms no election akidai hawana nia njema na chama hicho cha upinzani.

Amesema taifa limekuwa na mkwamo wa kisiasa kwa kuwa na chaguzi zisizo za huru na haki na wananchi kukosa fursa ya kushiriki chaguzi na kupata viongozi wanaowahitaji lakini sheria za uchaguzi sio rafiki hasa kwa vyama vya upinzani.

Mwakikuti anasema kutokana na ubovu wa sheria hizo CHADEMA imedhamiria kuzuia uchaguzi hivyo wanachama na viongozi wote wanapaswa kuunga mkono msimamo wa chama hicho badala ya kuibuka uraiani na kupinga licha ya kuwa na uhakika kuwa mifumo ya kiuchaguzi sio rafiki.

Kwa upande wake mwenyekiti wa BAWACHA mkoa wa Iringa bi. Suzana Mgonukulima, amesema kwa sasa wimbo wa kuimba ndani ya CHADEMA ni No reforms no election kwani kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na sheria na kanuni za uchaguzi zisizo rafiki ambapo kuanzia uchaguzi wa mwaka wa 2014 chaguzi zilianza kuvurugwa waziwazi.

Amesema wanawake wa mkoa wa Iringa wanaungana na kanda ya nyasa na wengine kote nchini ambao wamedhamiria kuunga kwa kauli moja msimamo wa CHADEMA Taifa wa kueneza kampeni hiyo kwa wananchi ili kutokufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutokana na chaguzi hizo kuonekana kama vita kwa ukweli kwamba watu mbalimbali wamebaki na makovu mabaya ya chaguzi hizo.

Pendo Mwashiuya ni Katibu wa BAWACHA mkoa wa Songwe na bi Sada Atick Adamu, wamesema wanaopinga kampeni ya No reforms no election ni watovu wa nidhamu kwani ukweli ni kwamba sheria za uchaguzi zilizopo zinapaswa kupingwa usiku na mchana na kupigania upatikanaji wa sheria rafiki za kiuchaguzi na agenda endelevu na agenda mama ya upatikanaji katiba mpya itakayozaa tume huru ya uchaguzi nchini Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!