Latest Posts

BIMA YA WASAFIRI ZANZIBAR YAZUA SINTOFAHAMU KWA WAGENI WAGONJWA, SERIKALI YAFAFANUA

Na Amani Hamisi Mjege.

Wazanzibari raia wa Uingereza wamejikuta wakikumbwa na mkanganyiko mkubwa kuhusu matumizi ya bima ya wasafiri (Inbound Travel Insurance) inayotolewa na Zanzibar Insurance Corporation (ZIC) baada ya kulazimika kulipia huduma za matibabu ambazo walidhani zingefidiwa kikamilifu na bima hiyo.

Matukio hayo yameibua maswali kuhusu ufanisi wa mfumo wa bima hiyo, ambao ulianza kutekelezwa rasmi Oktoba 1, 2024 kwa watalii na wageni wote wanaoingia Zanzibar kutoka nje ya Tanzania. Baba wa mtoto aliyepatiwa matibabu ameelezea masikitiko yake kuhusu huduma walizopata hospitalini.

“Sisi wageni wote tunaoingia Zanzibar, mgeni yeyote wa nje ya Tanzania, kwa Sheria ya Zanzibar iliyoanza tarehe 1 Oktoba 2024 anatakiwa alipe dola 44, mtoto chini ya miaka 10 dola 22 (takribani Shilingi za Kitanzania 60000). Sasa kama wageni wote wamekataa kuhusu kulipa hii kwasababu mgeni yoyote anayetoka nje anakuwa nayo bima ya afya tayari, kama sisi sote huwezi kusafiri kwenda nje unalipa bima ya afya, sasa malalamiko yetu ni kulipishwa mara mbili gharama za huduma ya afya, huku (Uingereza) unalipa bima ya afya, na ukifika Zanzibar unalazimishwa ulipe bima ya afya ambayo ni Dola 44 (Shilingi 120,000), matokeo yake unapelekwa hospitali halafu unafanyiwa vipimo na unaambiwa ulipie tena, sasa hatujui kwanini?”, amehoji.

Kwa mujibu wa Sheria mpya ya Zanzibar inayowalazimu wageni wote kulipa bima ya wasafiri, watalii wanaotembelea visiwa hivyo lazima walipie bima hiyo ili kupata kinga na huduma mbalimbali za dharura za matibabu wakati wa ziara yao. Hata hivyo, amelalamikia gharama walizotozwa baada ya bima hiyo kushindwa kufidia matibabu ya mwanawe.

“Nini faida ya hii insurance kwamba ina- cover kila kitu halafu unaambiwa ulipe tena? Mwanangu amekwenda kwenye holiday, na akaaambiwa hospitali ya Lumumba waliyotuambia tunapelekwa imejaa kwahivyo wakatupeleka kwenye hospitali nyingine na wakatuambia tulipe”, ameeleza.

Mama wa mtoto pia aliunga mkono malalamiko hayo, akisema walilazimika kulipa gharama zote licha ya kuwa na bima. “Mwanangu amefanyiwa hesabu, kalipa karibu laki moja elfu sabini, wakati tulinunua bima ya dola 22 kwa mtoto. Hakuna cha bure kama tulivyodhani,” amelalamika mama huyo.

Kulingana na gharama zote za matibabu kuanzia vipimo na tiba ambazo Jambo TV tumezipata kutoka kwa wahusika, ni Shilingi za Kitanzania 152,000.

Kwa upande wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), sintofahamu hiyo haikuwa jambo jipya. Meneja Biashara wa Shirika hilo, Hamida Juma, amefafanua juu ya sheria ya bima na taratibu zake. Ameeleza kuwa bima ya safari inakuwa na kiwango cha chini kinachoitwa excess – kiasi cha pesa ambacho mgeni anapaswa kulipia mwenyewe kabla ya bima kuanza kutumika.

“Bima yoyote ina kiwango kinachojulikana kama ‘excess,’ ambapo chini ya kiwango hicho, mteja anatakiwa kulipa mwenyewe. Kwa mfano, kwenye bima yetu ya wasafiri, kama gharama za matibabu ni chini ya dola 75 (Takribani Shilingi 204,638), mgeni anatakiwa kulipa mwenyewe. Matibabu yaliyotolewa kwa mtoto huyo yalikuwa chini ya kiwango hicho, ndiyo maana wazazi wake walitakiwa kulipa gharama hizo,” amesema Hamida.

Hamida ameendelea kueleza kuwa bima hiyo inalenga kupunguza matumizi mabaya ya huduma za bima na kuwahimiza watalii kuchukua tahadhari zaidi kuhusu afya zao na mali zao.

“Bima inachukua jukumu la kugharamia matibabu makubwa au ya dharura ambayo gharama zake zinazidi kiwango cha dola 75. Kama matibabu yalikuwa chini ya kiwango hicho, bima haiwezi kugharamia,” amefafanua na kuongeza,

“Hii ni tofauti na bima ya afya, hii ni ‘travel’. Kwenye bima ya afya ukiwa na kadi yake unakwenda hospitali, unaumwa macho, umefanya consultation (kumuona daktari) ukaandikiwa miwani, ukachagua frame, utaambiwa miwani hii ni 150000, lakini bima yako inagharamia mpaka 50000, zilizobaki analipa nani? analipa mgonjwa. Kwamba gharama za matibabu haya ili uanze kutibiwa ikiwa chini ya dola 75 utalipa mwenyewe, ikizidi 75 bima italipa hii tofauti”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, alitoa tamko rasmi mnamo Oktoba 17, 2024, akielezea kuwa lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha usalama wa watalii na wageni wote wanaoingia Zanzibar. Alisema kuwa serikali imeweka viwango vya kimataifa vya bima hiyo na inajitahidi kuhakikisha kuwa wageni wanafurahia huduma bora wakati wa kukaa kwao Zanzibar.

“Sheria hii inalenga kuimarisha usalama na kutoa huduma za matibabu kwa wageni wakati wa dharura kama ajali au magonjwa,” alisema Mkuya. Aliongeza kuwa kwa wale wanaoshindwa kukamilisha malipo ya bima kabla ya kuwasili Zanzibar, wanaruhusiwa kulipia bima hiyo mara wanapowasili.

Kuanzia Oktoba 1, 2024, Zanzibar ilianzisha sheria mpya inayotaka wageni wote wasiokuwa wakazi wa Tanzania kuwa na bima ya safari kabla ya kuingia kwenye visiwa hivyo. Bima hii inalenga kuwalinda wageni kwa kuwapa huduma za matibabu na kuwalinda na dharura mbalimbali, ikiwemo uokoaji na kupelekwa nyumbani iwapo hali itakuwa mbaya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!