Ili kukabiliana na utitiri wa ongezeko la taasisi za mikopo ambazo zimekuwa zikitoa huduma pasipo kuzingatia miongozo na sheria za utoaji mikopo kwa kuweka riba kubwa na zingine kufanyakazi pasipo kuwa na leseni, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua kampeni mahususi ya kutokomeza mikopo na taasisi hizo.
Akizungumza leo jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Zinduka usiumizwe kopa kwa maendeleo’ Meneja Msaidizi wa Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha BoT kutoka Makao Makuu Madogo ya Benki Dar es Salaam, Mary Ngassa amesema kampeni hiyo inalenga kuondoa mikopo ya kausha damu na mikopo umiza.
“Kampeni hii inalenga kuondoa mikopo umiza na kausha damu, mtu anakaushwa damu ama anaumizwa kwa kuwa hana uelewa, hajui wajibu wake na hajui nini cha kufanya anakuwa ana onewa kampeni hii inaenda kumwelimisha na kupanua uelewa wake kwenye masuala ya mikopo,” amesema
Mary ameongeza kuwa “Kampeni hii ya zinduka usiumizwe kopa kwa maendeleo itatembea hapa kwa Mwanza kwa muda wa siku 20 katika mitaa yote hasa ile ambayo tunaamini wakopeshaji wale ambao hawana leseni wapo na walaji wapo,”.
Akizungumza mara baada ya kuzindua kampeni hiyo Kaimu Mkurugenzi na Meneja Uchumi BoT Tawi la Mwanza, Isa Pagali amesema watakaobanika kutoa huduma za mikopo pasipokuwa na leseni watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Ukipatikana na hatia hiyo hukumu zipo wazi kama zilivyo ainishwa kwenye sheria ya huduma ndogo za kifedha za mwaka 2018 kifungu cha 16 ambapo atakaye hukumiwa anaweza kutozwa faini ya kati ya Milioni 20 hadi Milioni 100 au kufungwa jera kati ya miaka mitatu hadi mitano au vyote kwa pamoja hivyo tujiepushe na uhalifu huo”, ameeleza Isa.