Latest Posts

BOTI YA DORIA YA TRA KUIMARISHA UKUSANYAJI MAPATO NA USALAMA

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Mwenda, amesema mamlaka hiyo imejipanga kudhibiti magendo kupitia uzinduzi wa Boti ya Doria uliofanyika jijini Mwanza, Ziwa Victoria.

Bw. Mwenda amesema magendo yamekuwa yakihujumu uchumi wa nchi, kuathiri biashara halali, kuchochea uhalifu, na kuhatarisha usalama wa taifa, hivyo uzinduzi wa boti hiyo unalenga kukomesha vitendo hivyo.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Bw. Mwenda amebainisha kuwa boti hiyo itasaidia TRA kuokoa mapato yaliyokuwa yanapotea kutokana na ukwepaji wa kodi kupitia bidhaa za magendo, hasa vipodozi vinavyoingizwa kinyume cha sheria.

“Mbali na kukwepa kodi, vipodozi hivi vimekuwa vikiharibu afya za wananchi. Kazi yetu si kudhibiti mapato tu bali pia kulinda afya za Watanzania,” amesisitiza.

Kamishna Mkuu ameongeza kuwa uzinduzi wa boti hiyo unatilia mkazo usawa wa biashara kwa kuhakikisha kila mfanyabiashara analipa kodi.

“Wafanyabiashara wanaolipa kodi wanahitaji mazingira sawa ya ushindani. Wale wanaoingiza bidhaa za magendo wanauza kwa bei ya chini kwa sababu hawalipi kodi, jambo ambalo linakwamisha haki na usawa wa kibiashara,” amesema.

Aidha, Bw. Mwenda amewahamasisha wananchi kushirikiana na mamlaka hiyo katika vita dhidi ya magendo kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara haramu. Ameeleza kuwa TRA imetenga motisha kwa wananchi watakaofichua taarifa za wanaokwepa kodi, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni halali kisheria.

Kwa mujibu wa Bw. Mwenda, uzinduzi wa boti hiyo ya kisasa ni sehemu ya mkakati wa TRA wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha usalama wa nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!