Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga kimeeleza kusikitishwa kwake na kile ilichokiita “uporaji na uhalifu wa kiuchaguzi” uliofanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Aidha, chama hicho kimeeleza kuunga mkono maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA cha tarehe 02 Desemba 2024, na kusomwa na Mwenyekiti wa chama hichoTaifa, Freeman Mbowe, siku ya Desemba 10, 2024.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa, Emmanuel Ntobi, Jumatano Desemba 11, 2024 CHADEMA Shinyanga imeweka wazi hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo kuwahimiza wanachama na wananchi kuwanyima ushirikiano viongozi wa mitaa, vijiji, na vitongoji waliotajwa kuwa wametokana na uchaguzi ‘haramu’.
Aidha, chama hicho kimetoa wito kwa viongozi wake wa wilaya na majimbo kushirikiana na wadau mbalimbali wa kijamii, wakiwemo vyama vya siasa, taasisi za dini, makundi ya kiraia, na wananchi kwa ujumla, ili kupaza sauti za pamoja kudai mifumo huru ya uchaguzi na tume huru.
“CHADEMA Mkoa wa Shinyanga pia inasisitiza kuimarisha harakati za kudai Katiba Mpya, ambayo itaboresha mifumo ya sheria na uchaguzi nchini. Ni lazima Tanzania iwe na Tume Huru ya Uchaguzi itakayohakikisha uchaguzi wa kweli na haki,” ameongeza.
Mbali na hayo, chama hicho kimehimiza kuimarishwa kwa mfumo wa “CHADEMA Family” katika ngazi za chini ili kushirikiana katika masuala ya kijamii. CHADEMA pia imelaani vikali ukamatwaji wa viongozi na wanachama wake kabla, wakati, na baada ya uchaguzi, ikieleza kuwa hatua hizo zinalenga kudhoofisha demokrasia nchini.