Na Josea Sinkala, Mbeya.
Chama cha kutetea haki na maslahi ya walimu Tanzania (CHAKAMWATA) kimerudi tena kwa upya baada ya kukaa kimya kwa muda wa zaidi ya miaka mitano kutokana na kusitishwa kufanya kazi zake kutoka Serikalini ambapo kimeahidi kuendelea kupambania haki na maslahi ya walimu na watumishi wengine kote nchini.
CHAKAMWATA kimesema kitaendelea kutetea haki na maslahi ya walimu bila kuogopa licha ya kupitia misukosuko lukuki kwa muda mrefu kikiamini ndio chombo huru cha kuwatetea walimu.
Akizungumza na jamii hasa watumishi kupitia mkutano wake na waandishi wa habari jijini Mbeya, mwenyekiti wa chama hicho Taifa Mwalimu Ipyana Jackson, amesema kazi kubwa waliyonayo kwa sasa ni kuitafuta haki ya walimu anayodai imepokwa kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitano baada ya chama hicho kusitishwa kufanya kazi zake mwaka 2020 na msajili wa vyama vya wafanyakazi nchini.
Naye katibu mkuu wa Chama cha kutetea haki na maslahi ya walimu Tanzania (CHAKAMWATA) mwalimu Meshack Kapange, ameeleza kuwa baada ya chama hicho kushinda kesi yake ya rufaa ya kusitishwa kufanya kazi maamuzi yaliyotolewa na Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Februari 27 mwaka 2025, Chama kitaanza na kikokotoo cha wastaafu kwa kuwa ndipo walipoishia wakati msajili wa vyama vya wafanyakazi alipowafutia usajili mwaka 2020.
“Ndugu zangu nataka kuwaambia kikokotoo kile ni vita kati ya tajiri na masikini, kikokotoo ni vita kati ya watawala na watawaliwa, kikokotoo kile ni vita kati ya walioshiba na wenye njaa na wanataka kushiba kwahiyo hatukitaki”, amesema Kapange.
Viongozi wa CHAKAMWATA wamewaeleza waandishi wa habari kuwa chama hicho kilifutiwa usajili na msajili wa vyama vya wafanyakazi nchini bila kufuata utaratibu na hivyo kuwalazimu kwenda kudai haki yao mahakamani ambayo wameipata Februari 27 mwaka huu wa 2025 ambapo sasa kimerudi rasmi kwa ajili ya kuendelea kutetea haki na maslahi ya walimu na watumishi wengine pia.