Kufuatia vuguvugu linaloendeshwa kwa sasa na Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO) na Umoja wa Vijana Wasio na Ajira Tanzania(UYAM) wa kuitaka Serikali kushughulikia changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Chama cha Walimu na Wafanyakazi wa Shule zisizo za Serikali Tanzania (TPTU) kimejitokeza hadharani na kuishauri Serikali mambo 19 ya kufanya ili kutatua changamoto hiyo.
Akizungumza leo Machi 22, 2025 jijini Mwanza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa TPTU, Julius Mabula mbali na kudai chama hicho kinaunga mkono harakati hizo lakini pia ametahadharisha kwa kuita “harakati za wasomi ni mbaya” hivyo kutoa wito kwa Serikali na jamii kwa ujumla kutopuuzia.
Miongoni mwa mambo chama hicho kinashauri ni Serikali kuipa kipaumbele sekta binafsi, Serikali itatue changamoto ya mikataba na mishahala ya kazi kwenye ajira za sekta binafsi, waondolewe waajiriwa wote raia wa kigeni wasiohitajika na ambao hawana vibali halali vya kufanya kazi nchini lakini pia wazee wastaafu waondolewe kupisha vijana ambao hawana ajira na wapo mtaani.
“Lipo tatizo la wafanyakazi wengi raia wa kigeni na wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini, wameajiriwa na wanafanya kazi nchini, wameziba nafasi ambazo wazawa wangekuwa wameajiriwa, mathalani kwenye sekta ya elimu, zipo shule za binafsi nyingi zmeajiri raia wa kigeni wengi tu kama walimu, huku nchi yetu ina ziada ya walimu wa kutosha mtaani mpaka wanaisumbua serikali iwaajiri, raia wa kigeni ambao hatuna uhitaji wa ujuzi wao na hawana vibali vya kufanya kazi nchini waondolewe kuwapisha wazawa,” amesema.
Ameongeza kuwa “Watu wasio na sifa za kufanya kazi walizoajiriwa waondolewe pia kupisha watu wenye sifa za kazi hizo. Hii ni changamoto ambayo ipo kwenye ajira za sekta binafsi, kuajiriwa kwa watu wasiokuwa na sifa za kufanya kazi hizo walizoajiriwa, huku wenye sifa na kazi hizo kwa kuzisomea wameachwa wapo mtaani zipo shule nyingi tu zimeajiri walimu ambao ni kidato cha nne au kidato cha sita au watu waliosoma taaluma zingine,”.
Mabula amesema pia wanaitaka Serikali kuanzisha utaratibu wa kuwa na kanzidata ya wasomi wa taaluma zote waliohitimu ili waajiri wa sekta binafsi wawe wanaiomba Serikali wanapohitaji kuajiri na iwape kwa kutoa kibali cha kuajiri.
“Ili kurudisha heshima ya wasomi wetu nchini wa taaluma mbalimbali tunashauri Serikali sasa ianzishe kanzidata ya wasomi wetu wote wa taaluma zote nchini ambao wamehitimu masomo na hawajapata ajira, waajiri wawe wanaomba Serikalini wanapewa kibali cha kuajiri, watafanya usaili na watakaofaulu usaili wa waajiri wanaajiriwa hii itawaongezea thamani wasomi wetu mbele ya waajiri,” amesema.
Hata hivyo Mabula ameitaka Serikali ishirikiane bega kwa bega na vyama vya wafanyakazi nchini katika kuimarisha ustawi wa ajira nchini.
“Vyama vya wafanyakazi ni mkono wa tatu wa Serikali na vinafanya kazi kwa niaba ya Serikali hivyo ni afya zaidi Serikali kushirikiana navyo katika kuimarisha ustawi wa ajira kwa kuwa vyama vya wafanyakazi vipo kwa ajili ya kutetea haki za wafanyakazi si rahisi kuficha uovu wowote unaowaumiza wafanyakazi,”.