Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Pius Chatanda (MCC), ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, zoezi ambalo limeanza rasmi leo, Desemba 27, 2024, na litadumu hadi Januari 2, 2025. Chatanda amesisitiza kuwa zoezi hili ni muhimu kwa wananchi kutimiza haki yao ya kuchagua viongozi bora watakaosaidia kuleta maendeleo kwa watanzania.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Migori, Wilaya ya Iringa Vijijini, Chatanda alisisitiza kuwa kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura anapaswa kuhakikisha taarifa zake zimeboreshwa au kujiandikisha ikiwa bado hajafanya hivyo.
“Wito wangu kwenu ni kwenda kuboresha taarifa zenu katika daftari la mpiga kura. Wasiofanya hivyo watapoteza haki yao ya msingi ya kupiga kura,” alisema.
Chatanda alitoa wito maalum kwa wananchi wa mikoa ya Iringa, Mbeya, na Wilaya ya Mpwapwa, Dodoma, kujitokeza kwa wingi kujiandikisha. Alieleza kuwa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025 ni fursa muhimu ya kuchagua viongozi bora wenye uwezo wa kuleta matokeo chanya katika jamii.
Katika hotuba yake, Chatanda aliipongeza CCM Mkoa wa Iringa kwa juhudi zao za kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, juhudi ambazo zilipelekea mkoa huo kushika nafasi ya kwanza kitaifa. Alihimiza uongozi wa mkoa kuendeleza juhudi hizo ili kuhakikisha wananchi wanajiandikisha kwa wingi kwenye daftari la mpiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2025.
“Mkoa wa Iringa umefanya vizuri sana katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na ni muhimu kazi nzuri zaidi ifanyike kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mkuu,” alisema.
Chatanda alibainisha kuwa wananchi wote waliofikisha umri wa miaka 18 au wanaotarajia kufikisha umri huo mwakani wanapaswa kujiandikisha ili kushiriki uchaguzi mkuu. Alisisitiza kuwa kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kujiandikisha mwaka 2019/2020, sasa ni wakati wao wa kuhakikisha wanajitokeza.
“Ni muhimu vijana wetu wenye umri wa miaka 17 ambao mwakani watatimiza miaka 18 pia wajitokeze na kujiandikisha,” aliongeza.
Katika hotuba yake, Chatanda aliangazia juhudi za CCM za kuleta maendeleo nchini, akisema kuwa chama hicho kinaendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Alitoa mfano wa uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha dhamira ya dhati ya kuimarisha maisha ya wananchi kupitia miradi ya kijamii na kiuchumi.
“Ni jukumu letu kuunga mkono jitihada hizi kwa kuhakikisha tunajiandikisha na kuchagua viongozi bora wanaotokana na CCM,” alihitimisha Chatanda.