China imeishutumu Marekani kwa kutoa madai ya uongo kuhusu kuhusika kwake na biashara ya dawa haramu za fentanyl, ikisema kuwa Marekani inatumia kisingizio hicho kuhalalisha nyongeza ya ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka China.
Malalamiko hayo yamewasilishwa rasmi katika Shirika la Biashara Duniani (WTO), siku moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza ongezeko la asilimia 10 la ushuru kwa bidhaa kutoka China, akidai kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza biashara haramu ya fentanyl.
Katika kesi iliyowasilishwa WTO, China inasema ushuru huo ni wa kibaguzi na unalenga kulinda bidhaa za ndani dhidi ya ushindani wa kigeni, hali inayokiuka kanuni za biashara za kimataifa.
Hata hivyo, wataalamu wa biashara wanaonya kuwa China huenda ikashindwa katika kesi hiyo, kwani jopo linalohusika na utatuzi wa migogoro ndani ya WTO halifanyi kazi kikamilifu kwa sasa.
Trump amesema ongezeko la ushuru litalenga kuhamasisha kampuni za Marekani kutengeneza bidhaa zao ndani ya nchi, na kupunguza nakisi ya biashara baina ya Marekani na China.
Lakini hatua yake imezua wasiwasi wa kimataifa, huku wafanyabiashara na wawekezaji wakikosa uhakika wa soko, hali inayoweza kuathiri uchumi wa dunia.
Kampuni ya Sheertex, inayotengeneza nguo nchini Canada, imetangaza kupunguza wafanyakazi wake kwa asilimia 40 kwa muda, ikisema kuwa hali ya ushuru mpya imesababisha gharama kubwa za uzalishaji.