China imeapa kujibu vikali baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza ushuru mpya mkubwa kwa bidhaa zake zinazoingia Marekani, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya mageuzi makubwa ya sera ya biashara ya kimataifa ya Marekani.
Trump alitangaza ushuru wa asilimia 54 kwa bidhaa zote za China zinazoingia Marekani Jumatano, hatua inayotarajiwa kuibua mvutano zaidi kati ya mataifa mawili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani.
“China inapinga vikali hatua hii na itachukua hatua za kulinda haki na maslahi yake,” imesema Wizara ya Biashara ya China kupitia taarifa yake Alhamisi asubuhi.
Wizara hiyo imeelezea ushuru huo kama “mfano wa uonevu wa upande mmoja” na kuitaka Marekani kuondoa ushuru huo huku ikihimiza mazungumzo ya haki katika kutatua tofauti za kibiashara.
“Marekani imeamua kuweka ushuru huu kwa misingi ya tathmini zake binafsi na zisizo za haki, jambo ambalo linakwenda kinyume na kanuni za kimataifa za biashara na linadhuru haki halali za pande husika,” taarifa hiyo imesema.
Tangazo la Trump limeongeza ushuru wa asilimia 34 kwa bidhaa za China, juu ya ushuru wa asilimia 20 uliokuwepo. Tangu kurudi madarakani Januari, Trump tayari alikuwa ameweka ushuru wa nyongeza wa asilimia 10 katika awamu mbili, hatua ambayo Ikulu ya Marekani ilisema inalenga kudhibiti usafirishaji wa fentanyl (aina ya dawa) haramu kutoka China kwenda Marekani.
Trump ametangaza hatua hizo wakati wa hotuba katika bustani ya Rose Garden ya Ikulu ya Marekani, ambapo pia amefichua ushuru wa nyongeza wa asilimia 10 kwa bidhaa zote zinazoingia Marekani, huku mataifa ya Asia yakipigwa zaidi na ushuru huo mpya.
Kutokana na ushuru wa awali, baadhi ya kampuni za China zilihamishia uzalishaji wao katika mataifa mengine ya Asia ili kukwepa athari za kiuchumi. Hata hivyo, ushuru mpya wa Trump pia umeelekezwa kwa mataifa hayo: Vietnam itakabiliwa na ushuru wa asilimia 46, huku bidhaa kutoka Cambodia zikitozwa ushuru wa asilimia 49.
“Nina heshima kubwa kwa Rais Xi Jinping wa China na kwa taifa la China, lakini walikuwa wakitunyonya mno,” Trump amesema Jumatano. “Wanaelewa kilicho mbele yao… na watajitetea.”
Beijing tayari ilikuwa imetoa majibu ya wastani kwa ushuru wa awali uliowekwa na utawala wa Trump mwaka huu, ikijibu kwa ushuru wa asilimia 10 au 15 kwa bidhaa kama mafuta, mazao ya kilimo kama soya, ngano na kuku.
Aidha, China imeimarisha mbinu zake za kudhibiti usafirishaji wa madini muhimu pamoja na kulenga sekta na kampuni za Kimarekani kama njia ya kulinda maslahi yake.