Kufuatia changamoto ya walimu wanaojitolea shuleni kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutokulipwa mshahara au posho huku baadhi yao wakilipwa ujira mdogo ambao hautoshi kumudu mahitaji yao.
Shirika la Caring Pan African People in Africa (CPPA) nchini limekuja na mradi maalumu wa Mwalimu Hodari unaolenga kuwasaidia walimu wanaojitolea katika shule mbalimbali nchini kwanza kuwatambua lakini pia kuwapa posho ya Sh400,000 kwa mwezi itakayowasaidia kujikimu.
Akizungumza na Jambo TV Mkurugenzi wa Shirika hilo Bethel Zelothe amesema tayari mchakato wa kuwatambua walimu hao umeanza mkoani Mwanza katika Halmashauri nne ambapo mpaka sasa walimu wa kujitolea 867 wametambuliwa.
“Mpaka sasa hivi walimu ambao wapo kwenye programu hii ya Mwalimu hodari wapo 867 na hao ni wale wanaofundisha katika Halmashauri nne za Mkoa wa Mwanza za Sengerema, Magu, Ilemela na Jiji la Mwanza ambapo tumewafikia katika shule za msingi na Sekondari,” amesema.
“Walimu hao ni wale unakuta mwanzoni walikuwa wamekata tamaa lakini kwa mradi huu unaona kabisa matumaini yanaanza kuja, pamoja na kwamba wanawito wanapaswa wapate chochote kitu,” amesema.
Zelothe amesema mradi huo kwa sasa unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wafadhili na uungwaji mkono wa baadhi ya Mamlaka ya Serikali hali inayopelekea wao kushindwa kufikia lengo.
“Kwa upande wa mashirika kuna watu ambao walikuwa wamekubali kutusaidia tufanye nao shughuli hii lakini hapa katikati wamesita kutokana na matamko ambayo yametokea ya hivi karibuni ambayo yanatufanya sisi kushindwa kuelewa,” amesema.
“Mwanzoni tulikuwa tunajua kuanzia Machi mosi tungekuwa tumewakusanya wale walimu na kukaa nao na kuwapa semina elekezi lakini pia tuone kama tunaweza kuwapa chochote kile sasa mambo yaliyotokea hapa katikati wale wafadhili nao wamekunja mikono kidogo,” amesema Zelothe
Kutokana na hilo Zelothe ameiomba Serikali pamoja na wadau wengine kuwaunga mkono ili kufanikisha mradi huo wenye lengo la kuwasaidia walimu wanaojitolea shuleni kwa hiari.
Nao baadhi ya walimu wa kujitolea mkoani Mwanza wakizungumza na Jambo Tv wametaja changamoto ya fedha, idadi kubwa ya wanafunzi, kutokutambuliwa na kutoheshimika kuwa ni baadhi ya mambo wanayokumbana.
“Moja ya changamoto kubwa sana ni masuala ya kifedha mfano katika shule ambayo mimi nafundisha kidogo malipo ni changamoto ukizingatia pia ni shule ya kata ambayo pia haina miradi ambao unaweza kuzaliaha fedha kwa ajili ya malipo na hakuna kiwango cha moja kwa moja kwamba kila mwisho wa mwezi utapewa kiasi kadhaa ambacho ndo kusema ni mkataba hakipo,” amesema Rashidi Masindi, Mwalimu wa kujitolea katika moja ya shule ya Sekondari Jijini Mwanza.
Mbali na hoja hiyo kuungwa mkono na mwalimu mwenzake wa kujitolea, Innocencia Bruno pia ametaja changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi katika darasa moja kuwa inawafanya kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
“Shule nyingi za kata zina wanafunzi wengi sana hii inaathiri shughuli nyingi za ufundishaji hasa pale unapotaka kuwafanyia tathimini (assessment) wanafunzi lazima ufundishe na utoe kazi sasa unajikuta darasa moja lina wanafunzi 300 hadi 400 mpaka uje usahishe madaftari yao na kumaliza inachukua muda,” amesema.
Kwa upande wake mwalimu Faudhia Ponela ameitaja changamoto nyingine ya ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa wazazi lakini pia kudharaulika kuwa ni baadhi ya mambo wanayokumbana nayo.
“Ule ukaribu wa wazazi na walimu hasa sisi walimu wa kujitolea, wazazi wengi wanakuchukulia huyu anajitolea tu sio sawa na yule mwalimu ambaye ameajiriwa kidogo yeye ana hadhi kwa wazazi tofauti na sisi,” amesema Faudhia
Kutokana na changamoto hizo mwalimu Jackson John, Dotto Mazuyi na Happiness Michael wameiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la pili walimu wanaojitolea huku wakiamini endapo mradi huo ukipata ufadhili unaweza kuwa na mchango mkubwa kwao.