Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mheshimiwa Deusdedith Katwale amewaomba wakazi wa kata za Ntalikwa na Ndevelwa zilizopo manispaa ya Tabora kushiriki kwa wingi wao katika chaguzi za serikali za mitaa zinazotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Mheshimiwa Katwale amefafanua kuwa, zoezi hilo kabla ya Novemba 27,2024, ambayo ni siku ya kuwachagua wenyeviti wa mitaa ,Vijiji na Votongoji, kutatangulia mazoezi mengi humo katikakati, likiwamo zoezi muhimu la kujiandikisha kwenye orodha ya watakaopiga kura, ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 20 mwezi Oktoba mwaka huu, hivyo amewasihi wananchi kwenda kujiandikisha ili wapate fursa ya kuwachagua vongozi wao.
Mkuu wa Wilaya ametoa wito huo Septemba 25, 2024 katika ziara yake ya kikazi katika kata hizi mbili, ambapo mbali na wito huo wa uchaguzi, amekagua miradi ya maendeleo mathalani ameshiriki kusafisha eneo inapojengwa shule ya sekondari ya kata ya Ntalikwa ambayo aerikali imeleta milioni 603 kwa ajili ya ujenzi wake, amekagua ujenzi wa vyumba vitatu na ofisi moja vya shule shikizi ya Kitongoji cha Kikundi kilichopo kata ya Ntalikwa, kadhalika amekagua boma la bweni katika shule ya sekondari ya Ndevelwa.
Aidha, Mheshimiwa Katwale akiongea na wananchi wa Ntalikwa na Ndevelwa, mbali na wito wa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa,amewataka wananchi kufuata maadili ya Kitanzania, wasiwe wa kukurupuka na mila za kigeni zisizoeleweka, lakini pia jamii ishirikiane na serikali kuendelea kukemea matendo yasiyoyofaa kama ya ulawiti, ubakaji pamoja na kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu.
Halikadhalika, wananchi wa kata hizi wamepata fursa ya kueleza changamoto zao ambazo zilijikita kwenye sekta za maji, barabara, ardhi, na mifugo, ambapo Mheshimiwa Katwale akiwa ameambatana na wataalamu wa TANESCO, TUWASA, TARURA, pamoja na wataalamu kutoka manispaa ya Tabora, amejibu hoja na changamoto za wananchi hawa ,na changamoto ambazo zimeonekana zinahitaji muda na bajeti, amewaelekeza wataalamu wake hao kwenda kuzifanyia kazi kwa muda ambao ameelekeza.