Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewahimiza wakuu wa shule za sekondari wilayani humo kufanya kazi kwa ushirikiano, weredi, na hekima, huku wakizingatia kusimamia maadili ya wanafunzi shuleni ili kuboresha taaluma na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo kwa wakuu wa shule za sekondari za serikali, binafsi, maofisa watendaji wa kata 36, na wadau wa elimu, Mpogolo alisema serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha mazingira ya elimu kwa kiasi kikubwa kupitia ujenzi wa shule za kisasa na vifaa vya kufundishia.
Mpogolo amebainisha kuwa Rais Samia ametoa Shilingi bilioni 35 kwa Wilaya ya Ilala kwa ajili ya kuboresha sekondari, ikiwemo ujenzi wa shule za kisasa za ghorofa. Alisisitiza kuwa walimu wana jukumu kubwa la kuhakikisha ufaulu unaongezeka, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mpogolo ametoa wito kwa wakuu wa shule kuwashirikisha walimu wa kawaida katika masuala yanayosaidia kuinua taaluma badala ya kuwatenga. “Wapeni nafasi walimu hao kwa sababu mafanikio ya shule yanatokana na juhudi za pamoja,” amesema Mpogolo.
Akizungumzia maadili ya wanafunzi, Mpogolo amehimiza walimu kuchukua hatua za kudhibiti tabia hatarishi miongoni mwa wanafunzi, kama vile kubeba visu, mikasi, mawe, na bisbisi. Amependekeza ushirikiano na polisi wa kata ili kuhakikisha usalama shuleni.
Mpogolo pia amezungumzia changamoto za wazazi kulazimisha watoto wao kuhamishiwa shule maalumu bila vigezo stahiki. Amewasihi wakuu wa shule kutoa maelekezo sahihi kwa wazazi kuhusu taratibu za uhamisho.
Akihitimisha hotuba yake, Mpogolo amewapongeza walimu kwa juhudi zao na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuwajengea mazingira bora ya kazi kwa lengo la kuongeza ufaulu.
Awali, Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mussa Ally, alisema mafunzo hayo yalihusisha jumla ya washiriki 121 na yamelenga kuwakumbusha majukumu yao katika kuboresha taaluma shuleni.