Latest Posts

DCEA YAKAMATA KILO 37,197 ZA DAWA ZA KULEVYA KWA MIEZI MIWILI

 

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanikiwa kukamata jumla ya kilo 37,197.142 za dawa za kulevya katika kipindi cha Mei hadi Julai 2025, katika operesheni zilizofanyika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatano Julai 09, 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema dawa hizo zinajumuisha kilo 11,031.42 za Mitragyna Speciosa (dawa mpya ya kulevya inayotokana na mmea wa “Kratom”), bangi kilo 24,873.56, mirungi kilo 1,274.47, skanka kilo 13.42, heroin kilo 2.21 na methamphetamine gramu 1.42.

Lyimo ameeleza pia zilikamatwa dawa tiba zenye asili ya kulevya zikiwemo ketamine kilo 1.92, vidonge 1,000 vya Flunitrazepam (Rohypnol), pamoja na lita 6 za kemikali bashirifu aina ya hydrochloric acid. Katika kipindi hicho, ekari 1,045.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Mara, Kagera, Dodoma, Tabora, Morogoro na Arusha.

Aidha amesema, mamlaka hiyo ilizuia kuingizwa nchini kwa kilo 26 za heroin zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Msumbiji, huku jumla ya watuhumiwa 64 wakikamatwa kwa tuhuma mbalimbali zinazohusiana na biashara hiyo haramu.

Katika operesheni ya Temeke (bandari kavu), Kamishna Jenerali huyo wa DECA amesema, zilikamatwa kilo 11,031.42 za Mitragyna Speciosa zilizokuwa zimeingizwa nchini kutoka Sri Lanka. Dawa hizo zilifichwa ndani ya vifungashio vilivyoonesha kuwa ni mbolea.

Sambamba na hilo, ameeleza kuwa dawa hiyo ina kemikali aina ya Mitragynine na 7-Hydroxymitragynine (7-HMG) ambazo huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uraibu mkubwa pamoja na vifo vya ghafla.

Katika operesheni nyingine iliyofanyika eneo la Posta jijini Dar es Salaam, Lyimo amesema mamlaka hiyo iliwakuta raia wawili wa China — Chein Bai na Qixian Xin — wakisafirisha gramu 1.42 za methamphetamine, vidonge 1,000 vya rohypnol na ketamine kilo 1.92.

Katika eneo la Sinza, jijini Dar es Salaam, watu wawili walikamatwa kwa kuendesha kiwanda bubu cha kutengeneza biskuti zilizochanganywa na bangi na kuzisambaza katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara. Mkoani Lindi, mfanyabiashara wa madini naye alikamatwa akihusishwa na usambazaji wa aina hiyo ya biskuti.

Mamlaka pia imebaini kuwa baadhi ya wahalifu wameanza tena kutumia miili ya binadamu (maiti) kama njia ya kusafirisha dawa za kulevya, mbinu inayojulikana kama “begi.” Aidha, kuna ongezeko la raia wa kigeni kuwatumia Watanzania katika usafirishaji wa dawa hizo kupitia kampuni zao na vyombo vya usafiri kama bodaboda, bajaji, teksi na wasambazaji wa vifurushi.

Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali wa DECA, imewaonya wananchi kuwa waangalifu na mizigo wanayopewa au kuombwa kusafirisha kutoka kwa watu wasiowafahamu vizuri, kwani huenda ikawa sehemu ya usafirishaji wa dawa za kulevya.

Mamlaka hiyo imewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, ili tatizo hilo liondoke kabisa nchini. Imeelezwa kuwa yeyote atakayebainika kujihusisha na uzalishaji, usambazaji au biashara ya dawa za kulevya atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!