Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Tanzania Bara, Devotha Minja, Agosti 1, 2025, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea Ubunge katika Jimbo la Morogoro Mjini kupitia chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu katika Ofisi za CHAUMMA mkoani Morogoro, Minja amesema chama hicho kiko tayari kupambana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao na hakitasusia uchaguzi kama ambavyo baadhi wamekuwa wakidhani.

“CHAUMMA tupo imara, tumejipanga, na tutaingia kwenye uchaguzi kwa nguvu zote. Lengo letu ni kuhakikisha tunaleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi”, ameeleza Minja.
Hadi sasa, jumla ya wanachama nane wa CHAUMMA wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro, ikiwa ni ishara ya mwitikio chanya ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.