Naibu Mkuu wa Polisi anayekumbwa na shutuma nzito, Eliud Lagat, anatarajiwa kufika mbele ya Mamlaka ya Uangalizi wa Polisi Huru (IPOA) siku ya Alhamisi ili kuhojiwa kuhusu kifo cha mwanahabari maarufu Albert Ojwang’, aliyeaga dunia akiwa mikononi mwa polisi. Tukio hilo limesababisha hasira kubwa kitaifa na wito wa kuwajibika kwa maafisa wakuu wa polisi nchini Kenya.
Mwenyekiti wa IPOA, Isack Hassan, amethibitisha kuwa Lagat ameitwa rasmi kufika mbele ya mamlaka hiyo ili kurekodi maelezo yake. Tayari maafisa wa polisi zaidi ya 20, akiwemo Naibu Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nairobi Central (OCS), wamehojiwa. Aidha, IPOA imeomba rekodi za mawasiliano kutoka kampuni ya Safaricom kusaidia katika uchunguzi.
“DIG Lagat anatakiwa kufika mbele yetu kutoa maelezo na kuangazia uchunguzi huu. Tunawahakikishia wananchi kwamba hakuna mtu atakayefichwa. Haki itatendeka kwa wote”, amesema Hassan
Lagat amejiondoa kwa hiari kutoka katika majukumu yake wiki hii, akisema hatua hiyo imelenga kulinda heshima ya ofisi yake na kuruhusu uchunguzi huru na wa haki. Kupitia taarifa kwa umma, amesema “Nafanya haya kwa uamuzi wa kina na kwa kuzingatia maslahi ya umma. Niko tayari kushirikiana kikamilifu na uchunguzi huu.” Pia alitoa pole kwa familia ya Ojwang’.
Ojwang’, aliyekuwa bloga maarufu kwa kufichua madai ya ubadhirifu ndani ya jeshi la polisi, alikamatwa muda mfupi baada ya kuchapisha tuhuma nzito zinazomhusisha Lagat na ufisadi. Alidai Lagat alihusika na utoaji wa nafasi kimkakati ndani ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na vitengo vya trafiki ili kudhibiti mtandao wa mapato na ujasusi.
Kifo cha Ojwang’ kilichotokea baada ya kukamatwa, kimezua hasira na maandamano makubwa, huku Jaji Mkuu wa zamani David Maraga akimtaka Lagat akamatwe mara moja na kushtakiwa.
“Kuna ushahidi wa awali unaoonesha kwamba Bw. Eliud Lagat- moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja anahusishwa na kukamatwa, kuteswa, kunyongwa na hatimaye kuuawa kwa marehemu Albert Ojwang’,” alisema Maraga mbele ya wanahabari.
Mnamo Juni 11, Mkuu wa Jeshi la Polisi Douglas Kanja, akiwa mbele ya Seneti, alikiri kwamba uchunguzi wa ndani umeanzishwa baada ya taarifa kwenye mitandao ya kijamii kumhusisha Lagat na madai ya ufisadi pamoja na umiliki wa mali ya thamani ya dola milioni 2.6 huko Dubai.