Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Maulid J. Maulid alipokuwa akifunga mafunzo ya Walimu Wakuu 816 Mkoani Ruvuma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea Novemba 1, 2024.
Dkt. Maulid amesema, Walimu Wakuu wana jukumu la kufahamu maono ya Wizara zinazoshughulikia elimu ambazo ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na OR-TAMISEMI ambazo zinalenga kuhakikisha mtoto wa kitanzania anapata elimu bora itakayomjengea uwezo wa kujitegemea, hivyo ili kutimiza malengo hayo ni muhimu Walimu Wakuu kuhakikisha wanasimamia kwa weledi ufundishaji na ujifunzaji shuleni ili wanafunzi waweze kufikia ndoto zao.
“Sekta ya elimu ina jukumu la kuwaandaa Watoto ili kuleta maendeleo katika sekta zingine, hivyo Walimu Wakuu mkatekeleze zana ya uongozi bora kwa kuwasimamia walimu shuleni kufundisha kwa ufanisi unaotakiwa ili wanafunzi watimize ndoto zao”. Amesema Dkt. Maulid.
Nae, Afisa elimu Mkoa wa Ruvuma, Bi. Edith Mpenzile akizungumza na walimu wakuu hao amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya elimu hasa katika eneo la uboreshaji wa miundombinu ya elimu Mkoani Ruvuma. Mwl. Mpenzile amewasisitiza Walimu Wakuu hao kwenda kusimamia ustawi na usalama wa wanafunzi shuleni kwani Watoto wanapokuwa shuleni usalama na ustawi wao ni jukumu la mwalimu.
“Tukawe mfano na chanzo cha mabadiliko ya uongozi na usimamizi wa shule, tusimamie usalama na ustawi wa wanafunzi, nasisitiza tuipe taaluma kipaumbele lakini malezi ya watoto tusiache nyuma”. Amesema Mwl. Mpenzile
Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu-ADEM umeendesha Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu 816 wa Mkoa wa Ruvuma kwa siku tatu kuanzia tarehe 30 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba, 2024 yakilenga kuwajengea uwezo walimu wakuu kuhusu uongozi, usimamizi na uendeshaji fanisi wa shule katika halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma.
Hii ni awamu ya tatu ya mafunzo hayo ambayo yanafanyika katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Ruvuma ikihusisha jumla ya Walimu Wakuu 8,551 yakiendeshwa na ADEM chini ya mradi wa BOOST.