Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, ametoa fedha zaidi ya shilingi milioni 20 kwa ajili ya familia za wafiwa na majeruhi ambao wamelazwa kufuatia ajali ya gari iliyotokea Februari 25, 2025 mkoani Mbeya.
Akitoa salamu kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye zoezi la kuaga miili ya waliofariki katika ajali hiyo katika viwanja vya Uhindini jijini Mbeya, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya Patrick Mwalunenge, ameeleza kuwa mwenyekiti wa Chama hicho Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameagiza kila familia ya mfiwa ikabidhiwe shilingi milioni tano na shilingi milioni moja kwa kila aliyejeruhiwa kwenye ajali hiyo ili kuwasaidia kwenye matibabu.
Mwalunenge amemshukuru Dkt. Samia kwa kuomboleza pamoja na wafiwa na kuwahakikishia waombolezaji kuwa majeruhi wote watatibiwa chini ya usimamizi wa Chama hicho.
Naibu katibu mkuu wa CCM Tanzania bara John Mongela, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Dkt. Samia S. Hassan ameushukuru uongozi wa mkoa wa Mbeya kwa namna ambavyo umeshirikiana katika kipindi kigumu na juhudi ambazo zimefanyika katika kuokoa maisha ya majeruhi.
Amewashukuru pia bila kujali tofauti zao kuungana kuwasitiri waliofariki mkoani humo na kwamba ndio utamaduni wa kitanzania.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya mjini ambaye pia ni spika wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, amewasihi waombolezaji kuwa tayari wakati wote huku akiwaomba wananchi kuelekeza maombi yao kwa majeruhi ambao wamelazwa wakiendelea na matibabu ili wapone na kuendelea na majukumu yao.
Naye mwenyekiti wa wabunge wa mkoa wa Mbeya Mhe. Oran Njeza ambaye ni Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini amewasilisha salamu zake za rambirambi na kuwakilisha pia salamu za wabunge wa mkoa wa Mbeya akisema msiba huo ni mkubwa kwa mkoa na Taifa kwa kuondokewa na nguvu kazi hasa vijana.
Ikumbukwe mnamo February 25, 2025 ilitokea ajali ambayo ilihusisha magari mawili ambayo ni basi la kampuni ya CRN lenye namba za usajili T. 599 DZQ linalofanya safari zake kati ya Mbeya mjini na Mbarali (Ubaruku) na gari la Serikali aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili STM 6167 mali ya Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mbeya, baada kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu watatu papo hapo na kujeruhi wengine saba ambapo mwingine mmoja alifia hospitali hivyo jumla ya miili minne imeagwa tayari kwa maziko katika maeneo mbalimbali hapa nchini.