Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita, ambaye pia ni Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Kata ya Kalangalala, Richard Nzagamba, amewahimiza wahitimu wa Kidato cha Sita kutoka Shule ya Sekondari ya Mwatulole kutumia vyema elimu waliyoipata kwa manufaa yao binafsi na kwa maendeleo ya jamii.
Nzagamba alitoa wito huo wakati akimwakilisha Mgeni Rasmi, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Geita, Ndugu Magambo Nkilosubi, katika Mahafali ya Tatu ya Kidato cha Sita yaliyofanyika shuleni hapo.
Amesema kuwa ni muhimu kwa wahitimu hao kutumia maarifa yao kwa malengo chanya, ikiwemo kuchagua vyuo vitakavyowawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa pekee.
“Elimu mliyoipata ni silaha muhimu ya mafanikio. Itumieni kuleta mabadiliko chanya katika maisha yenu na kwa jamii inayowazunguka,” alisema Nzagamba.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi, walimu, wanafunzie pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na chama, na yalipambwa na burudani kutoka kwa wanafunzi na hotuba za hamasa kutoka kwa wageni waalikwa.