Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imepongezwa kwa juhudi zake katika kusimamia sekta ya maji nchini, huku ripoti mpya ikionesha mafanikio makubwa katika upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Katika hafla ya uzinduzi wa Taarifa ya 16 ya Tathmini ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira, iliyofanyika leo Machi 19, 2025 katika ukumbi wa Mlima City, Dar es Salaam, viongozi wa serikali na wadau wa sekta ya maji walieleza kuridhishwa na utendaji wa EWURA katika kuhakikisha huduma za maji zinaimarika.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amesisitiza umuhimu wa rasilimali ya maji kama zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ametoa rai kwa wananchi na mamlaka husika kushirikiana katika kulinda vyanzo vya maji na kutumia maji kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, ameeleza kuwa usimamizi wa sekta ya maji si kazi nyepesi, akifichua kuwa tangu aingie kwenye wizara hiyo mwaka 2017, amekutana na changamoto nyingi.
“Ukurugenzi si suti bali ni utendaji. Wakurugenzi wa mamlaka za maji wasiowajibika lazima wawajibishwe,” alisema Aweso.
Ameishukuru EWURA kwa kusimamia utekelezaji wa sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019, huku akisisitiza kuwa ripoti hizi hazipaswi kuwa za kawaida tu, bali ziwe chachu ya mabadiliko katika sekta ya maji.
Aidha, ripoti hiyo imebainisha kuwa mamlaka tano za maji zilizofanikiwa kudhibiti upotevu wa maji kwa kiwango cha juu ni Maganzo (4%), Nzega (6%), Kashiwasa (11%), Biharamulo (12%) na Mwanduzi (13%). Hata hivyo, changamoto bado zipo, kwani mamlaka kama Rombo (70%), Handeni (69%), Mugambo Kyabakari (64%), Ifakara (56%) na Kilindoni (55%) zimeorodheshwa miongoni mwa zilizo na upotevu mkubwa wa maji.
Akizungumza kwa niaba ya EWURA, Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Mark Mwandosya, ameeleza kuwa bajeti ya maendeleo ya sekta ya maji imeongezeka maradufu kutoka shilingi bilioni 206 mwaka 2010/2011 hadi shilingi bilioni 558 mwaka 2024/2025.
Amesisitiza kuwa uwekezaji katika sekta ya maji unachangia moja kwa moja kwenye maendeleo ya sekta ya afya, elimu na uchumi wa taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, amebainisha kuwa mamlaka hiyo imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019, ikiwemo tathmini ya utendaji wa mamlaka za maji kwa kuzingatia vigezo sita vikuu, ikiwemo upatikanaji wa huduma, viwango vya ubora, udhibiti wa upotevu wa maji, uendelevu wa utoaji huduma, hali ya kifedha na kuridhika kwa wateja.
Ripoti hiyo imebaini kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto za upotevu wa maji unaosababisha hasara ya shilingi bilioni 114.12 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Hata hivyo, Waziri wa Maji amesisitiza kuwa mamlaka za maji zinapaswa kuongeza juhudi katika kuboresha miundombinu na kupunguza gharama za uendeshaji ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia Watanzania wote kwa uhakika.
Kwa ujumla, uzinduzi wa ripoti hii umeonesha kuwa sekta ya maji nchini imepiga hatua kubwa, huku EWURA ikipongezwa kwa mchango wake katika kuhakikisha udhibiti wa huduma za maji unaimarika kwa manufaa ya Watanzania.