Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Oganaizesheni, Issa Usi Gavu, amepongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UWT Taifa, Mhandisi Fatma Rembo, kwa kuandaa futari ya pamoja iliyoleta mshikamano kati ya waumini wa dini zote, wakiwemo Waislamu na Wakiristo kwa lengo la kumuombea dua maalum Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya uongozi wake madhubuti .
Akizungumza katika hafla hiyo, Gavu amesema futari hiyo ni tendo la kiimani lenye baraka, ambalo limewaleta pamoja waumini wa Kiislamu na Wakristo, hasa kwa kuzingatia kuwa wote wapo katika kipindi cha toba na tafakuri ya kiroho.
Amesisitiza kuwa mshikamano wa kidini ni nguzo muhimu kwa amani na maendeleo ya taifa.
“Niwapongeze sana kwa mshikamano na upendo mliouonesha katika mwezi huu wa toba. Kufuturisha ni sadaka kubwa inayowaleta watu pamoja, na mmeonesha mfano mzuri wa mshikamano wa kweli kwa kumpongeza Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti unaoleta maendeleo, furaha, na amani nchini,” alisema Gavu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Yassin Mlowe, amesema tukio hilo limeonesha namna CCM inavyothamini mshikamano wa Watanzania bila kujali itikadi za kidini.
Ameeleza kuwa futari hiyo imetoa ujumbe mzito wa upendo na mshikamano ambao unapaswa kuendelezwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Naye, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UWT Taifa, Mhandisi Fatma Rembo, amesisitiza kuwa futari hiyo imeonesha jinsi Watanzania wanavyoweza kushirikiana kwa kuheshimiana na kusaidiana, bila kujali dini zao.
Amesema mshikamano kati ya waumini wa Kiislamu na Wakristo ni muhimu kwa mustakabali wa Taifa, na akahimiza wanawake wa CCM kushiriki kikamilifu katika kuendeleza umoja na mshikamano ndani ya jamii.
Nao wananchi wa Iringa walioshiriki katika futari hiyo wamepongeza juhudi za CCM Mkoa wa Iringa na Mhandisi Fatma Rembo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Utekelezaji UWT Taifa za kuimarisha mshikamano wa kidini, wakibainisha kuwa tukio hilo limekuwa darasa la kuimarisha amani na upendo katika jamii yao.