Michuano ya GEUWASA MAJI CUP 2025 imetamatika rasmi kwa mchezo wa fainali uliowakutanisha Tiger FC ya Geita Mjini dhidi ya CHAWASA FC kutoka Wilaya ya Chato. Mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la GGM lililopo mjini Geita ulimalizika kwa sare tasa ya 0-0 ndani ya dakika 90 za kawaida, na mshindi kupatikana kwa njia ya mikwaju ya penalti.
Katika mikwaju hiyo ya penati, Tiger FC waliibuka mabingwa baada ya kushinda kwa jumla ya penati 7–6, na hivyo kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mwaka huu wa 2025.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA), Frenk Changawa, ambao ndio waandaaji wa mashindano hayo, alisema kuwa michuano hiyo imeendelea kupata umaarufu mkubwa kila mwaka. Aliahidi kuwa katika mashindano yajayo, zawadi zitaongezwa ili kuyafanya kuwa na mvuto na thamani zaidi kwa washiriki.
Mgeni rasmi katika fainali hiyo alikuwa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Chato, Thomas Dime, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Geita. Katika hotuba yake, ameipongeza GEUWASA kwa kuandaa mashindano bora ambayo yameibua vipaji vingi vya vijana. Aidha, alitoa rai kwa waandaaji kuangalia uwezekano wa kuongeza aina nyingine za michezo katika mashindano yajayo, badala ya kujikita kwenye mpira wa miguu pekee.
Mashindano ya Geuwasa Maji Cup yamedumu kwa Takribani wiki nne yakizishirikisha jumla ya 14 ambapo ni makundi ya wanawake na wanaume pamoja na watoto kutoka kwenye Wilaya ya Geita Pamja na Chato.