Polisi Jamii Mkoani Geita wametakiwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi ili kutokomeza vitendo vya uhalifu katika maeneo yao na kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuimarika.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Polisi Jamii, CP Faustine Shilogile, wakati wa kampeni ya kuelekea kwenye Programu Maalum ya Polisi Jamii (Community Policing Outreach Program), inayodhaminiwa na Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita, Geita Gold Mining Limited (GGML).
“Tumeanzisha mpango huu wa Polisi Jamii kutokana na namna uhalifu ulivyokuwa umeshamiri kwenye jamii. Tunataka kila mwananchi awe sehemu ya suluhisho la ulinzi wa eneo lake.”Alisema Faustine Shilogile – Kamishna wa Polisi Jamii
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo amesema ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya GGML umelenga kuhakikisha uhalifu unapungua kwa kiwango kikubwa, sambamba na kutokomeza vitendo visivyofaa kwenye jamii.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, amewataka watendaji wa serikali za mitaa wakiwemo wa vijiji, mitaa na kata kuendelea kushirikiana na Polisi Jamii kwa lengo la kuhakikisha uhalifu unatokomezwa kabisa.
“Watendaji mnapaswa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na Polisi Jamii. Ulinzi wa maeneo yenu hauwezi kufanikishwa bila ushirikiano wa kweli kutoka kwa viongozi wa ngazi ya chini.”Alisema Mohamed Gombati – Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita
Mpango huu wa Polisi Jamii unaendelea kuleta matumaini ya kuimarisha usalama na mshikamano katika jamii, kwa kuwatambua wananchi kama sehemu muhimu ya mfumo wa ulinzi.