Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu ya Geita (GGML) imetoa msaada wa vifaa vya uchimbaji vyenye thamani ya shilingi milioni 24 kwa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Wanawake mkoani Geita (GEUWOMA). Sambamba na msaada huo, kampuni hiyo imetoa mafunzo maalum ya usalama wa mazingira kwa wachimbaji hao.
Meneja Mwandamizi wa GGML kitengo cha Uendelezaji, Gilbert Mworia, amesema kuwa mpango huo umeanza kwa kutoa mafunzo ya usalama mahali pa kazi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na Ofisi ya Madini.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa GGML Idara ya Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo, Dkt. Kiva Mvungi, ameeleza kuwa maeneo ya wachimbaji wadogo yanahitaji tahadhari kubwa kutokana na muingiliano mkubwa wa watu na vihatarishi vinavyoweza kusababisha madhara.
Ofisa Mkaguzi Mwandamizi kutoka OSHA, Amina Nangu, amesema sekta ya uchimbaji wa madini ina vihatarishi vingi, ambavyo vinaweza kuwa na athari kubwa endapo kanuni za afya na usalama hazitazingatiwa.
Katibu wa GEUWOMA, Mackrina Fabian, ameishukuru GGML kwa msaada huo, akisema kuwa utasaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji kwa wanawake na kuimarisha usalama wao kazini.
Mafunzo haya na msaada wa vifaa yanatajwa kuwa hatua muhimu katika kuinua uchimbaji salama wa wachimbaji wadogo, hususan wanawake, mkoani Geita.