Latest Posts

“HATUTAKI SIASA MADHABAHUNI”, GACHAGUA NA WENZAKE WAZUIWA KUHUTUBIA ANGLIKANA KWA MARA YA PILI

Kwa mara ya pili mfululizo, Kanisa la Anglikana la Kenya (ACK) limewazuia wanasiasa, akiwemo Makamu wa Rais wa zamani Rigathi Gachagua, pamoja na washirika wake na wale wa Rais William Ruto, kuzungumza mbele ya waumini wakati wa ibada.

Hatua hiyo ilichukuliwa wakati wa hafla ya kuwekwa wakfu na kuvikwa rasmi kwa Askofu Gerald Muriithi kama Askofu mpya wa Dayosisi ya ACK Mt. Kenya West, iliyofanyika katika Kanisa la St. Peter’s ACK, Nyeri Town.

Kama ilivyotokea Jumapili iliyopita, viongozi wa kisiasa walihudhuria hafla hiyo wakitarajia kupata fursa ya kutoa salamu za pongezi, miongoni mwao wakiwa Gachagua, wanasiasa wanaomuunga mkono Ruto, na Kiongozi wa Chama cha People’s Liberation, Martha Karua. Hata hivyo, hakuna aliyeruhusiwa kuhutubia waumini.

Mkuu wa Kanisa la ACK, Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit, amesisitiza msimamo wa kanisa la kuepuka siasa katika ibada. “Hata kama Rais angekuwepo, tungefanya hivyo hivyo kwa sababu tunataka ibada na madhabahu viheshimiwe”.

Ameongeza kuwa viongozi wa kisiasa wanaweza kuwasilisha ujumbe wao nje ya kanisa kwa kuwa “siyo sehemu ya ibada, bali ni sehemu ya mawasiliano ya kitaifa.”

Kwa mara nyingine, ACK imethibitisha msimamo wake wa kutoruhusu wanasiasa kutumia madhabahu yake kama jukwaa la kujipatia umaarufu wa kisiasa, ikisisitiza sera yake ya kutovumilia siasa kanisani.

“Si katika Kanisa la Anglikana. Tunaweza kuwa na mikutano ya amani nje, kwa sababu huwezi kujua lini mtu atasema jambo lisilofaa,” ameongeza Ole Sapit.

Baada ya kuzuiwa kuzungumza ndani ya kanisa, Rigathi Gachagua amepata fursa ya kuhutubia waumini nje ya kanisa, akitoa wito wa amani na mshikamano kwa wakazi wa Mlima Kenya kabla ya ziara ya Rais William Ruto katika eneo hilo.

“Watu wapendane. Watu waungane na kuwa wamoja. Tusikubali kuchochewa dhidi ya wenzao kwa sababu sisi ni wamoja,” amesema Gachagua.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!