Jumla ya wajawazito 71 na watoto 485 mkoani Mtwara wamepoteza maisha kutokana na changamoto mbalimbali za uzazi zilizojitokeza wakati wa kujifungua kwa mwaka 2023,2024
Akizunguza wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara (RCC) 2024 kilichofanyika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dkt. Benedicto Ngaiza amesema vifo hivyo vimetokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa kujifungua ikiwemo kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua kwa wajawazito.
Kwa upande wa vifo vya watoto wachanga sababu kubwa ikiwa ni pamoja na changamoto ya kujifungua wakati wa kuzaliwa, baadhi ya watumishi kukosa stadi ya kusaidia mtoto anaezaliwa ili kumuokoa.
Amesema ipo mikakati mbalimbali iliyowekwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa inapunguza vifo hivyo ikiwemo kutumia madaktari bingwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi, kufanya ufuatiliaji kujua sababu ili zisiweze kujirudia pamoja na kuimarisha usafirishaji wa dharura kwa wagonjwa kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa dharura (M-mama) unaosaidia kufuatilia uharaka wa rufaa.
Sambamba na hilo ameongeza kuwa kwa mwaka 2023,2024 jumla ya wananchi 217,195 walipima maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI na elfu 4,082 sawa na asilimia 1.8 wamegundulika na maambukizi ya Virusi vya ukimwi na kufanya kuwa na jumla ya wagonjwa waishio na VVU mkoa wa Mtwara ni 35,952.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Tunza Malapo amemuomba Mganga Mkuu wa Mkoa huo kuona namna ya kuweza kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kwani serikali imejitahidi kujenga miundombinu rafiki ya afya.