Taasisi ya Uhusiano wa Umma Tanzania (IPRT) imesaini makubaliano na Msajili wa Hazina Zanzibar kwa ajili ya uratibu wa pamoja katika kuandaa tuzo za umahiri katika mawasiliano ya umma Zanzibar yaani ‘Zanzibar Communication Excellence Awards (ZCEA)’ zinazotarajiwa kufanyika Julai 5 mwaka huu visiwani humo.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika mapema leo Machi 13, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo ilishuhudiwa Mkurugenzi wa IPRT,Dkt. Titus Solomon pamoja na Msajili wa Hazina Zanzibar, Bw Waheed Muhammad Ibrahim Sanya wakiwakilisha taasisi katika kurasimisha ushirikiano huo.
Akizungumzia hatua hiyo Dkt Titus alisema, makubaliano hayo yanalenga kuchochea uwezo miongoni mwa waandishi, vyombo vya habari na maafisa habari kwenye taasisi mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili waweze kutimiza wajibu wao kwa weledi na ufanisi unaokusudiwa.
“Ushirikiano huu na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar utakuwa ni chachu ya kuboresha mawasiliano kwa umma kuhusu utoaji wa taarifa mbalimbali zinazogusa maslahi ya umma zikiwemo taarifa zinazohusiana na miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa Zanzibar hususani miradi ya serikali katika kipindi cha miaka minne iliyopita,’’ alisema Dkt. Titus.
Zaidi, Dkt Titus alisema mpango huo utasaidia kuvijengea uwezo vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla utakaowasaidia kubainisha changamoto zinazoikabili jamii na miradi hiyo ili serikali iweze kuchukua hatua kwa wakati.
“Tuzo hizi pia zinalenga kuwahamasisha wadau wa habari kujenga uwezo kwenye maeneo mahsusi (specialization), hivyo kutoa mchango mkubwa zaidi kwa jamii.’’ Alisema Dkt Titus huku akibainisha kuwa uzinduzi wa tuzo hizo utafanyika hivi karibuni Zanzibar ambapo waandaaji watafafanua maeneo mahsusi (category) ambayo wadau hao wa habari wataweka mkazo ili kuwa kwenye nafasi ya kujishindia tuzo na fedha.
“Ifahamike kwamba kabla ya uzinduzi huu, waandishi wa habari na watangazaji watachagua maeneo ambayo watayaangazia (specialization) ili wapate mafunzo mahsusi kabla. Kufanikisha hili, mialiko kuhusu mafunzo haya itatumwa kwenye vyombo vya habari mapema iwezekanavyo.’’ Aliongeza.
Dkt Titus alielezea matumaini kuwa ushirikiano huo utaleta tija kubwa na kutoa hamasa zaidi kwa wadau wa habari, vyombo vya habari pamoja na maafisa habari wanaohudumu kwenye taasisi za umma Zanzibar na hivyo kuboresha mawasiliano baina ya taasisi zao na umma.
Akielezea wasifu mfupi wa taasisi hiyo ya IPRT Dkt Titus alisema imekuwa ikitoa mafunzo maalum kuhusu mawasiliano ya kimkakati na utawala bora kwa taasisi za umma na binafsi Tanzania Bara na Zanzibar huku akitaja baadhi ya taasisi zilizonufaika na mafunzo hayo kuwa ni pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania ambapo maofisa zaidi ya 1,600 wamepatiwa mafunzo.
“Taasisi nyingine ni Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA),Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS), Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),Norwegian Church Aid, Chama cha Walimu Tanzania (CWT),Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya (Bara na Visiwani) na Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC).’’ Alitaja.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina Zanzibar, Bw Waheed Muhammad Ibrahim Sanya alisema kuwa ana matumiani makubwa kuwa tuzo hizo zitaleta mapinduzi makubwa kwa maendeleo ya Zanzibar kupitia uchocheaji wa utoaji wa taarifa sahihi na zenye weledi kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali visiwani humo kwa faida ya umma.
“Tumejiridhisha kwamba wenzetu wa IPRT wameandaa mipango mikubwa ambayo itasaidia kuboresha utendaji kwa wadau wetu muhimu ambao ni waandishi wa habari pamoja na maafisa habari kwenye mashirika ya umma ambao ndio wamekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali,’’ alisema
Zaidi Bw Sanya alielezea pia kuhusu mpango wa taasisi hizo mbili katika utoaji wa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati na utawala bora kwa viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali visiwani humo.
Akizungumzia tuzo hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Bw Juma Burhan Mohamed aliwapongeza washirika hao wawili kwa uamuzi wa kuanzisha tuzo hizo kwa wadau wa habari, hatua ambayo alisema itasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa habari sahihi zenye kuzingatia weledi wa taaluma ya habari.
“Umma unapofikiwa na taarifa sahihi hususani kuhusu miradi inayotekelezwa na serikali yao inakuwa jambo bora zaidi hata kwa serikali yenyewe na viongozi wake kwasababu wanakuwa kwenye nafasi ya kupata mrejesho wenye uhalisia kutoka kwa wananchi na wanakuwa kwenye nafasi ya kuzifanyia kazi taarifa hizo kwa haraka na kwa kuzingatia uhalisia wake…naipongeza sana Ofisi ya Msajili Hazina Zanzibar na IPRT,’’ alibainisha Bw Mohamed.



