Israel imerejea mashambulizi makali dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, hatua ambayo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameielezea kama “mwanzo tu” wa operesheni mpya ya kijeshi.
Katika taarifa ya video aliyotoa Jumanne usiku, Netanyahu amesisitiza kuwa “mazungumzo yataendelea tu chini ya mashambulizi,” akionesha kuwa mpango wa kumaliza vita haupo mezani kwa sasa.
Mashambulizi hayo ya anga yalilenga maeneo mbalimbali, ikiwemo Beit Lahia, Rafah, Nuseirat na Al-Mawasi, huku jeshi la Israel likisema limevipiga malengo muhimu vya Hamas. Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imeripoti kuwa zaidi ya watu 400 wameuawa na mamia kujeruhiwa. Haya ni mashambulizi makubwa zaidi tangu usitishaji wa mapigano ulipoanza Januari 19.
Katika tamko rasmi, Misri, ambayo imekuwa mpatanishi katika mazungumzo ya amani, imelaani mashambulizi hayo, ikiyaita “ukiukaji wa wazi” wa makubaliano ya kusitisha mapigano na hatua inayohatarisha ustawi wa eneo hilo. Tamim Khallaf, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, amesema kuwa mashambulizi haya yanaongeza hatari kwa hali ya usalama wa kanda hiyo.
Israel inasema kuwa mashambulizi hayo yamewaua watu muhimu wa Hamas, wakiwemo Meja Jenerali Mahmoud Abu Watfa, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Gaza na afisa wa ngazi ya juu wa usalama wa kundi hilo.