Latest Posts

JAMES ADAIWA KUJERUHIWA NA BOMU LA POLISI, POLISI YAJA NA KAULI TOFAUTI

Hali ya sintofahamu imetanda katika Kijiji cha Kirungu, Kata ya Janda wilayani Buhigwe, kufuatia tukio lililosababisha James Mkunde (24), dereva bodaboda, kujeruhiwa vibaya mguuni, huku askari polisi mmoja akiumizwa jicho na gari la polisi kuharibiwa. Tukio hilo lililotokea Machi 20, 2026, limeibua malalamiko ya matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya polisi, huku jeshi hilo likidai lilikuwa likijihami dhidi ya kundi lililojichukulia sheria mkononi.

Diwani wa Kata ya Janda (CCM), Shaaban Ahmad, ametoa simulizi inayodai kuwa vurugu hizo zilianza baada ya raia mmoja kuhoji utaratibu uliotumiwa na polisi kumkamata binti mmoja raia wa Burundi anayeuza bia. Diwani anadai mwananchi aliuliza kama tajiri wa binti huyo ana taarifa za kukamatwa kwake, jambo lililozua mzozo wa maneno na polisi.

“Sasa mmoja kati ya wananchi akauliza akamuuliza askari ‘sasa unamkamata huyu binti tajiri yake ana taarifa?’, Kwahiyo baada ya kuwa amemuuliza hivyo tayari yeye (polisi) akamwambia wewe unatuuliza hivyo kama nani? yule mwananchi akamwambia ‘mimi ni mwananchi tu wa kawaida, naona tu niulize hivyo’, yule askari akamuuliza ‘sasa unatufundisha kazi?’, ameeleza Diwani huyo alipozungumza na Jambo TV jana akibainisha kuwa polisi watatu walijaribu kumuingiza mwananchi huyo (aliyehoji) kwenye gari kwa nguvu.

James Mkunde (mdogo wa mwananchi huyo) alipotoka nyumbani kuja kuuliza kulikoni, alipigwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu la machozi au kishindo mguuni kabla hata ya kuwafikia askari.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma (SACP), Filemon Makungu, ametoa picha tofauti leo akisema askari walikuwa katika doria ya kawaida ya “kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu” na walimkamata mtuhumiwa wa kuishi nchini kinyume cha sheria. Kamanda Makungu anabainisha kuwa kundi la watu lilijitokeza na kuzuia askari wasiondoke na mtuhumiwa na kwamba askari walishambuliwa kwa mawe na silaha za jadi, na kupelekea kioo cha mbele cha gari la polisi (Toyota Landcruiser) kuvunjwa.

Amesema kuwa askari mmoja amejeruhiwa jicho la kushoto, na James Mkunde amejeruhiwa mguu wa kulia kati ya goti na unyayo.

Kwa mujibu wa Diwani wa Janda, James Mkunde kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Maweni akiendelea na matibabu baada ya kupewa huduma ya kwanza katika zahanati ya kijiji. Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa uchunguzi wa kina unafanyika ili kubaini waliohusika na fujo hizo na uharibifu wa mali ya serikali.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma linatoa wito kwa Wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuendelea kutii sheria bila shuruti na kutojihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi”, ameeleza Filemon.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!