Jamii mkoani Mtwara imetakiwa kuwa tayari kupokea elimu wanayopatiwa na wataalamu wa afya hususani wamama wajawazito na wale waliotoka kujifungua.
Hayo yamezungumzwa na Mratibu wa Huduma ya Mama na Mtoto wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (DRCHCO), Somoe Moa kwenye kikao cha uchambuzi wa vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga kwa robo ya tatu kuanzia Januari hadi Machi 2024.
Amesema katika kipindi hicho kuna kifo kimoja cha mama kilichotoka na uzazi ambapo wataalamu wanaendelea kutoa elimu itakayomsaidia mama mjamzito katika kipindi chote hadi siku ya kujifungua.
‘lakini pia jamii imekuwa ikipeana elimu tofauti ambayo imekuwa ikileta changamoto kwa wajawazito hao hivyo tunaiomba jamii iwe tayari kupokea ambayo wataalamu tunasema”
“Sisi wataalamu tunatoa elimu lakini wakienda kwa jamii wanaiga kutokana na stori wanazopena hususani kutokuwahi kwenye kituo cha afya unapohisi uchungu hilo sio jambo zuri ni vema ukaja kwenye kituo kama kufanyiwa uangalizi ufanyiwe kwenye vituo vya huduma za afya.”amesema Moa
Ametoa rai kwa jamii hiyo, kuwahi mapema kwenye vituo vya afya pindi tu wanapojihisi kuwa na ujazito na kufuatilia rufaa walizopewa na wataalamu hao ili kutoleta madhara wakati wa kujifungua.
“Jamii iwahi mapema kwenye vituo vinavyotoa huduma lakini pia tunapotoa rufaa naomba zile rufaa wazifuatilie kwa wakati, unaweza kwenda kliniki ambayo haitoi huduma ya yultrasaundi lakini ukapewa rufaa kwenda kituo jirani ila walio wengi hawafati”amesema Moa
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Abeid Abeid amewataka wataalamu hao kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya huduma ya afya ya uzazi, mama na mtoto kwa kufuata taratibu zote.
Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo, Joel Tiho amesema lengo la kikao hicho ni kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati thabiti itayopunguza vifo visivyokuwa vya lazima.