Latest Posts

JAMII YAHAMASISHWA KUENDELEA KUWASAIDIA WATOTO YATIMA

Watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu wapatao 150 mkoani Mtwara wamepatiwa msaada wa mahitaji mbalimbali ili kuwafanya nao waweze kusherehekea sikukuu ya Iddy kwa furaha kama watoto wengine.

Msaada huo umetolewa na wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Baraza la Mashekhe Mkoa wa Mtwara katika zoezi lililoratibiwa na Katibu wa Baraza hilo ambaye pia ni Mratibu wa Watoto Yatima na Wanaoishi katika Mazingira Magumu, Abdul Hafidhi Kilindi.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa msaada huo, Kilindi amesema lengo la zoezi hilo ni kuwaletea tabasamu watoto hao kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo kanzu kwa wavulana, vitambaa vya kushona kwa wasichana, fedha kwa ajili ya mashono, nguo za ndani, soksi pamoja na viatu.

Amesema pamoja na juhudi hizo bado watoto hao wanahitaji msaada zaidi ikiwemo majuba na mahitaji mengine ya sikukuu, hivyo ametoa wito kwa jamii kuendelea kuwasaidia ili kuwafanya wajisikie kuthaminiwa na jamii inayowazunguka.

Aidha amemuomba Mungu awajaalie watoto hao maadili mema ili wakue wakiwa watu wema watakaoweza kuwajali wengine katika jamii.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wanawake Waislamu Mkoa wa Mtwara, Aisha Suleiman, amesema baraza hilo limeamua kujikita katika kusaidia malezi ya watoto hao kutokana na changamoto wanazokutana nazo baadhi ya wanawake wanaobaki na watoto baada ya baba kufariki.

Amesema juhudi hizo pia zinalenga kuhamasisha wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia watoto hao kwani kutoa ni tendo la moyo.

Naye mmoja wa wadau walioshiriki katika utoaji wa msaada huo, Nasra Muhamed, amesema aliamua kushiriki zoezi hilo kwa kutambua kuwa watoto hao wanahitaji msaada huku walezi wao wakiwa na uwezo mdogo wa kuwahudumia.

Ameitaka jamii kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha watoto hao wanapata mahitaji muhimu ya maisha.

Akitoa shukrani kwa niaba ya watoto wenzake, Abubakar Shabani amewashukuru wadau wote waliotoa msaada huo huku akisema bado wanahitaji msaada zaidi na kuiomba jamii kuendelea kuwasaidia na kuwawakumbuka.

Aidha imeelezwa kuwa yeyote atakayeguswa na wito huo anaweza kutoa mchango wa aina yoyote kwa ajili ya kusaidia watoto hao kupitia namba 0783814051 (Abdulhafidh K. Kilindi).

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!