Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba amesema Kiongozi wa Chama cha National Unity Platform (NUP) Robert Kyagulanyi Ssentamu Bobi Wine ameanzisha vita na taifa lake hivyo kwa namna yoyote ni lazima wamkamate.
Kupitia mtandao wa X Muhoozi amechapisha akisema kuwa amesikia kuwa Bobi Wine amejificha chini ya choo lakini kwa namna yoyote ile atakamatwa na kuwajibishwa.
“nimesikia Kabobi(Bobi Wine) anajificha chini ya choo, ameanzisha vita na nchi ambayo sasa hivi anajaribu kuikimbia atalipia kila kitu alichofanya” amesema Muhoozi
Ameongeza kuwa haijalishi Bobi Wine yupo ndani ya nchi au lah kwa namna yoyote na kwa faida ya maslahi ya kiusalama na Jumuiya ya Madola inabidi afungiwe kufanya siasa kabisa.
Muhoozi amesisitiza kuwa “Kuanzia sasa, mtu yeyote atakayemtangaza Robert Kyagulanyi (maarufu kama Bobi Wine) kuwa kiongozi wake wa kisiasa lazima afutwe”
Bobi Wine mwenyewe amedai kuwa kwa sasa yupo mafichoni baada kudai kuwa anatafutwa na majeshi ya nchi hiyo kwa kile alichoeleza kuwa wamedhamiria kumtesa.