Kamati ya ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro (RCC) imeazimia kutokuligawa Jimbo la Moshi Vijijini kutokana na kutokukidhi baadhi ya vigezo vinavyohitajika na Tume ya Uchaguzi (INEC)
Kamati ya ushauri ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu imekutana na kufanya Kikao hicho cha kujadili kugawa Jimbo la Moshi Vijiji Machi 28,2025 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa ambapo baada ya mjadala mrefu kiliazimia kutokugawa Jimbo hilo kutokana na vigezo kutokukidhi kama inavyotakiwa.
Akiwasilisha taarifa ya kugawa Jimbo hilo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Shadrack Mhagama ameeleza kuwa Kamati ya ushauri ya Wilaya (DCC) ilijulishwa kuwa Baraza la Madiwani lilijadili na kupendekeza kuligawa Jimbo hilo na kuafiki ugawaji huo uhusishe jimbo la Moshi vijijini na siyo Jimbo la Vunjo.
Amesema kuwa Kamati ya ushauri ya Wilaya baada ya kupitia maoni ya Wananchi,mjadala na maoni ya Kamati ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Kamati ya fedha, uongozi na mipango,Baraza la Madiwani lilipendekeza mgawanyo wa majimbo usigawanye Jimbo la Vunjo kwasababu Wananchi katika Jimbo hilo walishaanza mchakato wa kuanzisha Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Ameongeza kuwa Baraza la Madiwani lilipendekeza Jimbo la Moshi Vijijini lenye jumla ya wakazi 281,530 Kata 16 na Vijiji 79 Jimbo hilo ligawanywe kuwa na majimbo 2 ikiwemo Jimbo jipya la Mawenzi ambalo litakuwa na jumla ya watu 111,650 kutokana na sensa ya watu na malazi ya Mwaka 2022 ukubwa wa eneo Km za mramba 197.636864 na kuundwa na Kata 7 za Arusha Chini,Kundi,Kibosho Magharibi,Okaoni, Kibosho Kati,Kibosho Mashariki na Kirima ziunde Jimbo la Moshi Magharibi na jimbo hilo kuwa na Vijiji 34.
Amesema kuwa Jimbo la Moshi Vijijini lingebakiwa na Jumla ya watu 169,880 kutokana na sensa ya watu na malazi 2022 ukubwa wa eneo Km za mraba 228.956186 litaundwa na Kata 9 ikiwemo Mabogini,Mbokomu,Old Moshi Mashariki,Old Moshi Magharibi, Kimochi,Uru Mashariki,Uru shimbwe,Uru Kaskazini na Uru Kusini Ziunde Jimbo la Moshi Vijijini na kuwa na Vijiji 45.
Itakumbukwa kuwa uzingatiwaji wa vigezo vilivyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi inahitaji kigezo Cha watu kuwa 400,000 kwa Kila jimbo ambapo majimbo yote yaliyotakiwa kugawanywa hayana idadi ya kigezo kinacho hitajika.
Vigezo vingine ni hali ya jiografia, Mawasiliano, Hali ya kiuchumi,ukubwa wa eneo,mipaka ya Kiutawala,Idadi ya wabunge, Mpangilio wa makazi na uwezo wa ukumbi wa Bunge.
Kufuatia uchambuzi wa vigezo hivyo Wajumbe waliochangia walipendekeza kusiwepo na ugawaji wa jimbo hilo kwa sasa kutokana na kutokukidhi vigezo vingi na kuepuka kufanya mambo kisiasa.