Kufuatia tukio la kuanguka, jengo la ghorofa mbili katika eneo la magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, ameziagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kufika mara moja eneo la tukio na kushirikiana na timu za wataalam kutoka mamlaka nyingine za serikali kupata sababu za kuanguka kwa jengo hilo na kuchukua hatua stahiki kwa wale wote ambao watabainika kukiuka sheria za kitaaluma katika ujenzi na usimamizi wa jengo hilo. Hatua hizo zilichokuliwa na Waziri Bashungwa, zinakuja kufuatia taarifa za mwanaume mmoja ambaye ni fundi wa ujenzi aliyefahamika kwa jina moja la Omary maarufu Mwarabu aliyefariki dunia huku mafundi wenzake wanane wakijeruhiwa baada ya jengo la ghorofa mbili ambalo walikuwa wanaendelea kulijenga kuporomoka April 17, 2024 katika mtaa wa Magogoni wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam.