Shughuli ndogondogo zimeripotiwa kuanza kurejea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kufikia saa 1 asubuhi ya Jumatano, baada ya mgomo wa wafanyakazi uliofanyika usiku wa kuamkia siku hiyo kusababisha usumbufu mkubwa.
Kulingana na taarifa ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA), mgomo huo uliotangazwa na wafanyakazi wa uwanja huo ulisababisha ucheleweshaji na taharuki kwa abiria na mashirika ya ndege.
Mkurugenzi Mkuu wa KAA Henry Ocoye, katika taarifa kwa vyombo vya habari alithibitisha kuwa juhudi zinaendelea kurejesha huduma kwa ukamilifu. “Tunaendelea kushirikiana na wadau muhimu ili kurejesha shughuli za kawaida. Tunaomba radhi kwa usumbufu uliotokea na tunathamini uvumilivu wa abiria katika kipindi hiki,” alisema Ocoye.
KAA iliwashauri abiria kuwasiliana na mashirika yao ya ndege ili kuthibitisha hali ya safari zao, kwani mgomo huo ulikuwa bado unavuruga ratiba za ndege.
Mgomo huo, uliosababishwa na mpango wa serikali wa kukabidhi usimamizi wa JKIA kwa kampuni ya India, Adani Group, kwa miaka 30, umesababisha hasira na maandamano. Picha zilizotumwa mitandaoni zilionesha abiria wakijaribu kuchukua mizigo yao katika uwanja huo wakati mgomo ulipoanza.
Mpango wa kukodisha uwanja huo kwa Adani Group kwa malipo ya dola bilioni 1.85 umekosolewa vikali, huku wakosoaji wakidai kuwa utasababisha upotevu wa ajira kwa wafanyakazi wa ndani na kupunguza mapato ya walipa kodi kwa miaka ijayo.
Kulingana na Citizen Digital, JKIA ni moja ya viwanja vya ndege vyenye shughuli nyingi zaidi barani Afrika, ikihudumia abiria milioni 8.8 na tani 380,000 za mizigo mwaka wa 2022-23. Serikali ya Kenya imejitetea kuwa mpango huo ni muhimu ili kuimarisha miundombinu ya uwanja huo, ikiwamo kuongeza njia ya pili ya kurukia ndege na kuboresha eneo la abiria.