Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, amewahutubia wafuasi wake baada ya uchaguzi, akikaribishwa kwa shangwe huku wimbo wa Beyoncé Freedom ukichezwa, ambao ulikuwa sehemu ya kampeni yake.
Harris ameanza kwa kusema kwamba “moyo wake umefurahi” na amejaa shukrani kwa imani ambayo wafuasi wake wameonesha kwake na kwa nchi. Amekiri kuwa matokeo ya uchaguzi hayaendani na matarajio yake, lakini akawahakikishia wafuasi wake kwamba “nuru ya Marekani itang’aa kila wakati mradi tu tusikate tamaa na tuendelee kupigana.”
Akiendelea, Harris amewashukuru wanafamilia wake na kuwatambua watu waliomsaidia, wakiwemo mume wake, Doug, pamoja na Rais Joe Biden na mke wake Jill, na mgombea mwenza wake Tim Walz na familia yake.
Makamu wa Rais ametumia hotuba hiyo kueleza lengo kuu la kampeni yake, ambalo lilikuwa la kujenga jumuiya na umoja wa kitaifa. Amesema kuwa timu yake iliongozwa na upendo kwa Marekani na shauku ya kujenga mustakabali bora wa taifa.
Katika ujumbe wake kwa Wamarekani wote, Harris amewakumbusha kuwa kuna mambo mengi zaidi yanayowaunganisha kuliko yale yanayowatenganisha. Ametoa wito wa kukubali matokeo ya uchaguzi na kuheshimu misingi ya demokrasia, akisema kwamba “kanuni ya msingi ya demokrasia ni kukubali matokeo,” ambayo ndiyo inayotofautisha mfumo wa demokrasia na udhalimu. Harris amethibitisha kuwa amewasiliana na Donald Trump na kumpongeza kwa ushindi wake, akiahidi kushiriki katika mchakato wa uhamishaji wa madaraka kwa amani.