Kamanda wa kundi la mamluki la Urusi ameuawa nchini Mali kufuatia shambulio la wapiganaji wa waasi wakati wa dhoruba ya mchanga, kundi hilo limeeleza.
Utawala wa kijeshi katika jimbo hilo la Afrika Magharibi uligeukia kundi la Wagner mwaka 2021, kutafuta uungwaji mkono katika kupambana na vikosi vya jihadi na wanaotaka kujitenga.
Siku ya Jumatatu kundi la Urusi ambalo sasa limejigeuza kuwa kundi linaloitwa Africa Corps yaani Kikosi cha Afrika lilisema limejiunga na jeshi la Mali katika vita vikali dhidi ya waasi wanaotaka kujitenga na wanamgambo wa jihadi wiki iliyopita.
Kulingana na Shirika la Habari la BBC, watu wanaotaka kujitenga walifanya shambulizi kubwa, na kuua takriban mamluki 20 hadi 50.
Vile vile, wanablogu kadhaa wa kijeshi wa Urusi waliripoti kwamba takriban watu 20 waliuawa katika shambulio la kuvizia karibu na mji wa kaskazini-mashariki wa Tinzaouaten.
Katika taarifa rasmi iliyotumwa kwa Telegram, kundi la mamluki la Urusi halikubainisha ni wanajeshi wangapi waliofariki, lakini walithibitisha kupata hasara. Hii ni pamoja na kamanda, Sergei Shevchenko, ambaye aliuawa wakati wa makabiliano.
Hapo awali mamluki hao walielezwa kuwaangamiza waislamu wengi na kuwafanya wengine kukimbia.