Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Elibariki Kingu amesema jamii imekuwa ikikumbwa na maradhi kama UKIMWI, Homa ya Ini pamoja na magonjwa ya ngono, hivyo serikali inatakiwa kuweka mipango ya kutenga fedha za ndani ili kupambana na magonjwa hayo.
Ameyasema hayo kwenye kikao cha 6 mkutano wa 18 Bunge la 12, tarehe 4 Februari 2025 Bungeni wakati akiwasilisha Taarifa za Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, na Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI.
“Licha ya jamii kukumbwa na maradhi ikiwemo UKIMWI, Homa ya Ini pamoja na magonjwa ya ngono, hivyo basi Bunge limeazimia kutenga fedha za ndani kwaajili ya kupambana na magonjwa hayo kwa kuongeza kasi ya utoaji elimu”, amesema Elibariki.
Aidha amesema Bunge linaazimia kutoa kipaumbele cha kuajiri wahudumu wa sekta ya afya ili matibabu yaweze kutolewa kwa ngazi zote.
“Kwa kuwa sekta ya afya inakabiliwa na upunguvu wa rasilimali watu katika vituo vya kutolea afya nchini kwa kiwango cha asilimia 55, na kwa kuwa imekuwa ikiathiri sana nchini, Bunge linaazimia serikali itoe kipaumbele cha kuajiri wahudumu wa afya ili huduma za afya zitolewe nchini kote”, amesema Elibariki.
Aidha Kingu ameishauri Serikali kuwekeza katika hospitali za ndani ili kupunguza gharama za kuendesha matibabu, pamoja na ujenzi wa majengo mengine.