Kamati za ulinzi na usalama ngazi ya wilaya na kata wamepewa mbinu tano za namna ya kushughulikia matukio ya uhalifu na wahalifu kabla na baada ya kutokea katika jamii.
Mbinu hizo zimetolewa kwenye mafunzo ya elimu ya ulinzi na usalama kwa viongozi na wataalamu wa ngazi za wilaya na mamlaka za Serikali za Mitaa zilizofanyika wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Akitoa mafunzo hayo kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya na watendaji wa kata, Mkufunzi wa Elimu ya Uraia na Utawala Bora kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, ASP Iddah John Ringo amesema kwanza wanatakiwa kufahamu kila kona ya maeneo ya wanayoongoza huku pia wakihakikisha wanakuwa na wasiri wa kuwapatia taarifa ya kinachoendelea.
“Wanatakiwa kama watendaji wa kata kuhakikisha wanaifahamu vizuri mitaa yake katika masuala ya ulinzi na usalama kwa maana ya awe na watoa taarifa kutoka kwenye kila eneo la kata yake ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa utoaji wa taarifa kwa maana ya watendaji wa vijiji au vitongoji,” amesema.
ASP Ringo amesema pia wanatakiwa kuhakikisha wanashiriki katika matukio au shughuli za kijamii ili kunasa taarifa za uhalifu na wahalifu kabla au baada ya kutokea kupitia minong’ono au mazungumzo ya wananchi.
“Watendaji wa kata wajue wanawajibu wa kushiriki katika matukio na shughuli mbalimbali za kijamii ili kujiweka karibu na watu lakini pia yatamsaidia kupata taarifa ambazo zinaweza kumsaidia kuondoa majanga ya uhalifu kabla hayajatokea” amesema.
Hata hivyo pia amewataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na watendaji wa kata kuhakikisha wanatunza siri za watoa taarifa huku wakihakikisha wanashughulikia matukio yote yasiyo ya kawaida yanayotokea katika maeneo yao.
“Tunawaomba wakuu wa vyombo na watendaji wa kata wanavyopewa zile taarifa basi mafriji yao yagandishe wawe na tabia ya kuwalinda wasiri wao wasitoe taarifa ya wasiri wao kwa sababu kwanza wanatengeneza uhasama wa mtoa taarifa na mashtakiwa au mtuhumiwa”
“Na hii inasababisha wale wenye nia nzuri ya kutoa taarifa zitakazosaidia kupambana na majanga ya kihalifu kukaa kimya na kusababisha suala dogo kugundulika likiwa kubwa hali itakayopelekea Serikali kutumia gharama au nguvu kubwa lakini kumbe wangepata taarifa za mwanzo wangezibiti mapema”
Ameongeza kuwa “mfano unaweza kukuta kuna mauaji yanayotokea katika eneo lako namna ambavyo wale wanavyouawa ni namna ambayo inafanana na imelenga kundi moja anaposhuhudia mauaji hayo yanajirudia anapaswa kutoa taarifa”
Afisa kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Peter Dihoko anesema kiongozi mzuri ni yule anayehakikisha kuwa ana mifumo mizuri ya kupata taarifa na kushughulikia matukio kwa wakati.
“Kiongozi mzuri ni yule anayehakikisha mgeni yoyote anayeingia katika eneo lake la mamlaka anahakikisha anamtambua na anaweka mifumo mizuri ya kupata taarifa,” amesema Dihoko.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ludigija amewataka watendaji wa kata kutumia taratibu za utawala bora katika kushughulikia migogoro ya kijamii.
“Leo tumepata elimu katika eneo la usalama lakini pia tumefundishwa ukamataji sahihi manayake tunapoenda kutekeleza majukumu haya tusiseme hilo halinihusu,” amesema Ludigija.
Mtendaji wa Kata ya Nkalalo, Salum Mussa Salum ametoa shukrani kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwapa mafunzo hayo.
“Nitoe shukrani za dhati kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutupatia mafunzo haya kwa sisi watendaji wa kata kwani ni muda mrefu hatujapatiwa mafunzo kama haya,” anesema Salum.
Naye Mtendaji wa Kata ya Shilembo, Marietha Mushi, amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuboresha utendaji kazi wa watendaji wa kata.
“Tunaamini mafunzo haya yanaenda kuwa na matokeo chanya, tumeshakumbushwa wajibu wetu na namna ya kuwajibika mbele ya wananchi,” amesema Mushi.