Saa chache baada ya Sudan kutangaza hatua kali dhidi ya Kenya kwa kukaribisha wanamgambo wa RSF jijini Nairobi kwa mkutano wao, serikali ya Kenya imejitokeza kutetea msimamo wake katika kusaidia kutatua mgogoro wa Sudan.
Kupitia taarifa rasmi kutoka kwa Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri na Wizara ya Mambo ya Nje, Kenya imeeleza kuwa haijakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa, misingi ya Umoja wa Afrika wala Mkataba wa Kuzuia Uhalifu wa Kimbari kama inavyodaiwa na Sudan.
Ikionekana kutetea uwepo wa RSF jijini Nairobi, Kenya imesisitiza kuwa ni jambo la kawaida kwa mataifa yanayokumbwa na migogoro kuruhusu pande zinazohasimiana kufanya mikutano ya amani katika nchi jirani ili kufikia suluhu ya kudumu.
“Msimamo wa Kenya uko wazi: tunatoa nafasi ya mazungumzo, bila kuchukua upande wowote, kwa sababu tunaamini katika uwezo wa mazungumzo ya amani kutatua mizozo ya kisiasa,” ilisema taarifa hiyo.
Serikali ya Kenya imeeleza kuwa lengo lake ni kutoa fursa kwa RSF pamoja na mashirika ya kiraia ya Sudan kujadili na kutafuta njia ya kurudisha utawala wa kiraia nchini humo. Tamko hilo limetaja kuwa Kenya inaamini suluhu ya haraka na endelevu inaweza kupatikana kwa njia ya mazungumzo badala ya harakati za kijeshi.
Zaidi ya hayo, Kenya imetambua athari kubwa za mgogoro huo kwa raia wa Sudan na hivyo imeahidi kutoa dola milioni 2 kusaidia kupunguza janga la kibinadamu linaloikumba nchi hiyo.
Wakati huohuo, wanamgambo wa RSF wanatarajiwa kutoa tamko rasmi kwa wanahabari baada ya kuthibitisha kuwa watatia saini makubaliano ya kuunda serikali mbadala ndani ya Sudan. Makubaliano hayo yanatarajiwa kufanyika Ijumaa hii jijini Nairobi.
Kenya imekumbusha kuwa mwaka 2002 ilifanikisha mazungumzo ya amani yaliyomaliza vita vya kiraia Sudan kupitia Mkataba wa Machakos, na kwa msingi huo imependekeza kuwa mgogoro wa Sudan hauwezi kusuluhishwa kwa njia ya kijeshi, bali kupitia majadiliano.