Latest Posts

KENYA YAZUIA KUONESHWA MAKALA YA BBC YA MAUAJI YA WALIOANDAMANA

Mamlaka za Kenya zimezuia kuoneshwa kwa makala ya uchunguzi ya BBC “Blood Parliament”, ambayo inaangazia mauaji ya waandamanaji yaliyofanywa na polisi mbele ya jengo la Bunge la Kenya mwaka jana, shirika hilo la Uingereza limethibitisha.

Filamu hiyo ilikuwa ipeperushwe Jumatatu jioni katika jumba la sinema la Unseen Nairobi, ikifuatiwa na mjadala wa wataalamu. “Tulilazimika kughairi maonesho ya ‘Blood Parliament in Kenya’ kutokana na shinikizo kutoka kwa mamlaka,” alisema msemaji wa BBC.

“Tumesikitishwa sana na hali hii. Hata hivyo, watazamaji bado wanaweza kuitazama kwenye chaneli ya BBC Africa Eye kwenye YouTube.”

Maandamano ya Juni na Julai 2024 dhidi ya Muswada wa Fedha na serikali ya Rais William Ruto yaliongozwa na vijana wa kizazi cha Gen-Z. Zaidi ya watu 60 wanaripotiwa kuuawa baada ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi katika miji mbalimbali.

Hadi sasa, hakuna uchunguzi wa wazi uliowasilishwa kuhusu utovu wa nidhamu wa polisi.

Filamu hiyo ya BBC, ambayo ilitazamwa zaidi ya mara milioni mbili kwa siku moja tu kwenye YouTube, inamtaja afisa Job Kaboi wa Kituo Kikuu cha Polisi Nairobi akiwahamasisha wenzake kuwaua waandamanaji.

Afisa mwingine, aliyefunika uso wake, anaaminika kuwawinda na kuwapiga risasi David Chege (39) na Erickson Mutisya (25) nje ya majengo ya Bunge. Aidha, filamu hiyo inamhusisha mwanajeshi wa KDF na kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Eric Shieni (26), aliyepigwa risasi kichwani wakati akikimbia.

Ripoti hiyo imeibua wito mpya wa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka maafisa wote waliohusika katika mauaji hayo.

Kwa upande wao, Mamlaka ya Kusimamia Polisi Huru (IPOA) imesema imekamilisha uchunguzi wa kesi 22 kati ya 60 zinazohusiana na vifo vilivyotokea. Kesi nyingine 36 bado zinaendelea kuchunguzwa, mbili zipo mahakamani, mbili zimefungwa kwa maamuzi ya ndani, tatu zilifungwa kufuatia maelekezo ya DPP, na nne ziko ofisini kwa DPP.

Mwenyekiti wa IPOA, Issack Hassan, amesema wamepokea taarifa za majeruhi 233 waliotokea katika maandamano hayo, lakini uchunguzi unasuasua kutokana na kutokushirikiana kwa polisi na mashahidi.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen, anatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo Jumanne hii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!