Na. Mwandishi Wetu
15 Januari, 2025
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kwela, Sumbawanga Mkoa wa Rukwa Mhe. Deus Sangu amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mwl. Missana Kwangura kuanza rasmi kupokea wanafunzi wa shule ya Sekondari Kilangawana katika jimbo hilo.
Mhe. Sangu ametoa maelekezo hayo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Kilangawana, Jimbo la Kwela katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
“Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini sana elimu, ndiyo mana ikaamua kujenga shule hii ya Sekondari ya Kilangawana ili kuwasaidia na kuwapunguzia Watoto adha ya kusafiri umbali mrefu wakitafuta elimu” alisema Mhe. Sangu.
Aidha, ameelekeza viongozi wa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kushirikiana na wananchi wa Kata ya Kilangawana kuhakikisha Watoto wote wanaotakiwa kusoma katika shule hiyo ya Sekondari Kilangawana wanafika shuleni na kuendelea na masomo kama ilivyopangwa.
Katika mkutano huo Mhe. Sangu ameahidi kuongeza madawati, kuleta walimu na kufuatilia kwa karibu fedha za kuongeza madarasa na ujenzi wa vyumba vya maabara.