Kiongozi Mkuu wa kundi la Hamas la Palestina Ismail Haniyeh ameelezwa kuuawa mapema asubuhi ya siku ya Jumatano nchini Iran kwa mujibu wa Hamas ambayo imeeleza kuwa shambulizi hilo ni kama “njia ya kuamsha mapigano mapya”.
Walinzi wa Mapinduzi ya Iran wamethibitisha kifo cha Haniyeh saa chache baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa nchi ya Iran na kusema kuwa wanachunguza zaidi, hata hivyo hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa mamlaka ya Israeli na Ikulu ya Marekani kwa mujibu wa Shirika la habari la Reuters.
Habari hizo, ambazo zilikuja chini ya saa 24 baada ya Israel kudai kumuua kamanda wa Hezbollah ambapo Israel ilisema ndiye aliyehusika na shambulio baya katika milima ya Golan inayokaliwa na Israel, zinaonekana kurudisha nyuma uwezekano wa makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano huko Gaza.
“Mauaji haya yaliyofanywa na Israel kwa ndugu Haniyeh ni ongezeko kubwa ambalo linalenga kuvunja dhamira ya Hamas,” afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri aliiambia Reuters. Amesema Hamas itaendeleza njia iliyokuwa ikifuata, na kuongeza “Tuna uhakika wa ushindi”.
Haniyeh, ambaye kwa kawaida anaishi Qatar, amekuwa uso wa diplomasia ya kimataifa ya kundi la Palestina wakati vita vilivyoanzishwa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7 vikipamba huko Gaza, ambapo wanawe watatu waliuawa katika shambulio la anga la Israel.
Akiwa ameteuliwa kushika wadhifa wa juu wa Hamas mwaka 2017, Haniyeh amekuwa akiishi kati ya Uturuki na mji mkuu wa Qatar Doha, akitoroka njia za usafiri za Ukanda wa Gaza uliozingirwa na Israel na kumwezesha kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya kusitisha mapigano au kuzungumza na mshirika wa Hamas ambaye ni Iran.