Latest Posts

KIPINDI CHA MVUA SI MUAFAKA KWA UTENGENEZAJI WA BARABARA – MENEJA TARURA

 

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Tarime, Charles Marwa, amesema kuwa kipindi cha mvua si muafaka kwa utengenezaji wa barabara kwani kufanya hivyo ni sawa na kuharibu barabara au kuongeza ukubwa wa tatizo.

Akizungumza na Jambo TV jana, Machi 25, 2025, alisema kuwa mvua ni moja ya vyanzo vikuu vya uharibifu wa barabara, hivyo kufanya ukarabati wakati wa msimu huo huleta changamoto kubwa na huweza kuzidisha matatizo badala ya kuyatatua.

Kauli hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu baadhi ya barabara za mijini na vijijini kuharibika kiasi cha kuwa ngumu kupitika, huku nyingine zikifungwa kabisa kwa vyombo vya moto.

Marwa alieleza kuwa moja ya changamoto zilizochangia hali hiyo ni ucheleweshaji wa mikataba ya matengenezo ya barabara. Alifafanua kuwa kwa sasa TARURA inatekeleza bajeti ya 2023/2024, ambayo ilipaswa kutekelezwa mapema, huku bajeti ya 2024/2025 ikiwa haijaanza kutumika. Pia, aliongeza kuwa mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana hadi Januari 2025, na mvua zinazoendelea Machi mwaka huu, zimekuwa changamoto katika utekelezaji wa miradi ya barabara.

Kuhusu malalamiko ya wananchi kuhusu barabara ya Mtaa wa Rembiri, Marwa alisema kuwa barabara hiyo ni mpya na ilibidi ichimbwe ili kuboresha mfumo wa maji. Kuhusu korongo lililopo kwenye barabara hiyo, alieleza kuwa TARURA liliweka korongo hilo kwa ajili ya kusafirisha maji, lakini kutokana na utelezi uliopo msimu huu wa mvua, barabara hiyo inahitaji kuwekewa changarawe ili kurahisisha matumizi yake.

Aidha, alitaja sababu nyingine zinazosababisha uharibifu wa barabara kuwa ni uvunjifu wa sheria za barabarani, ikiwemo wakulima kulima hadi ndani ya mitaro ya kupitisha maji, hali inayosababisha mitaro kuziba na maji kuhamia barabarani, hivyo kuharibu miundombinu.

“Mimi nikikuta mtu amelima hadi kwenye mitaro ya maji, huwa nang’oa mazao yake kwa sababu ni kosa kisheria. Maji yanapotakiwa kupita kwenye mitaro iliyozibwa, hujielekeza barabarani na kuharibu miundombinu,” alisema Marwa.

Aidha, aliwaomba maafisa mipango kuhakikisha wanatoa semina kwa wenyeviti wa mitaa kuhusu namna ya kuibua vipaumbele vyao na muda muafaka wa kuwasilisha maombi yao ili kuepusha ucheleweshaji wa bajeti.

“Mimi ningeshauri hawa watu wa mipango wawe wanawapa semina wenyeviti ili wajue namna ya kuibua vipaumbele vyao kwa wakati. Mfano, mwezi huu kuna mmoja ameleta ombi lake la barabara wakati ambapo bajeti tayari ipo Dodoma, hivyo atalazimika kusubiri hadi bajeti ijayo,” alisema Marwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!