Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe imetoa ujumbe maalum kuelekea msimu wa Sikukuu ya Krismasi na kuukaribisha mwaka mpya wa 2025.
Katika taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ameeleza masuala mawili muhimu yanayohusu maendeleo ya mkoa huo, ambayo ni udumavu kwa watoto na ukatili wa kijinsia pamoja na mauaji.
Kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Afya, Demografia na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022, Mkoa wa Njombe unaongoza nchini kwa kiwango cha udumavu, ambapo asilimia 50.4 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanakabiliwa na tatizo hilo.
Hali hiyo inatajwa kuwa changamoto kubwa inayoathiri ukuaji wa mwili na akili ya watoto, na hivyo kuchangia matokeo duni shuleni pamoja na uwezo mdogo wa uzalishaji mali kwa watu wazima.
Serikali ya Mkoa, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeanzisha kampeni yenye lengo la kupunguza udumavu kwa kaulimbiu “Kujaza Tumbo si Lishe, Jali Unachomlisha.”
Kampeni hiyo inahimiza matumizi ya vyakula mchanganyiko, kutoa elimu kwa akina mama kuhusu lishe bora wakati wa ujauzito na kunyonyesha, pamoja na ufuatiliaji wa ukuaji wa watoto kupitia vituo vya afya.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa juhudi hizi zinatokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha tatizo la udumavu linatokomezwa.
Lengo la Mkoa wa Njombe ni kufikia viwango vya udumavu vinavyokubalika kimataifa ifikapo mwaka 2030.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameeleza masikitiko makubwa kuhusu ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia na mauaji ndani ya Mkoa wa Njombe kwa mwaka 2024.
Vitendo hivyo vimeelezwa kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyosababisha majeraha ya kimwili na kisaikolojia kwa waathirika, huku vikiwa vinachafua taswira nzuri ya mkoa huo.
Wananchi wamehimizwa kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili mapema kupitia namba za dharura kama vile 119 kwa Polisi na 0738 68 24 34 ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Viongozi wa kisiasa, kidini, na kijamii pia wametakiwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu madhara ya imani potofu, visasi, na ukosefu wa maadili.
Katika juhudi za kukabiliana na tatizo hilo, Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa vyombo vya dola vitachukua hatua kali dhidi ya wote wanaojihusisha na ukatili wa kijinsia na mauaji.
Aidha, jamii imehimizwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kujenga mazingira salama na yenye maadili bora kwa watoto na familia kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa ametoa pole kwa familia zilizoathiriwa na matukio ya ukatili na mauaji, huku akisisitiza kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha matukio hayo hayajirudii tena.
Vilevile, amewakumbusha wananchi umuhimu wa lishe bora na mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, na magonjwa ya moyo.
Kwa kumalizia, Mkuu wa Mkoa wa Njombe amewatakia wananchi wote wa mkoa huo heri ya Krismasi na Mwaka Mpya 2025, akisema kwamba ana imani kubwa kuwa kwa kushirikiana, Mkoa wa Njombe utafanikiwa katika juhudi za kupambana na udumavu, ukatili wa kijinsia, na mauaji.