Latest Posts

KUNDI LA WHATSAPP LA JAMBO TARIME LILIVYOLETA FARAJA KWENYE MAISHA YA PETER

Kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp, Jambo Tarime, limeadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa msaada wa kiti mwendo kwa mmoja wa wanachama wao, Peter Baraka, mkazi wa Wilaya ya Tarime. Hafla hiyo ilifanyika nyumbani kwa Peter na kuhudhuriwa na viongozi na wanachama wa kundi hilo.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya kundi, Kiongozi wa Jambo Tarime, Emmanuel Segere, alisema kuwa lengo la kundi hilo ni kusaidia wenye uhitaji kama sehemu ya mchango wao kwa jamii.

“Tunasherehekea miaka kumi ya kundi letu. Tumekuwa tukifanya hafla kila mwisho wa mwaka na kutoa mahitaji mbalimbali kwa wahitaji. Leo tumeamua kusaidia mwanakikundi mwenzetu ambaye amekuwa na changamoto ya ulemavu,” amesema Segere.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Matiko, ambaye pia ni mwanachama wa kundi hilo, amesisitiza umuhimu wa makundi ya kijamii kusaidia wenye uhitaji na kujenga uwezo wa kiuchumi. Matiko ameahidi kusomesha mtoto wa Peter kupitia Matiko Foundation, akisema:

“Mtoto wa Peter atapata elimu bora hadi atimize ndoto zake. Pia, kwa kuwa Peter anapenda mpira, nitagharimia kisimbuzi kwa muda wa mwaka mzima ili apate burudani anayopenda.”

Peter Baraka, akipokea msaada huo, ametoa shukrani kwa wanachama wa Jambo Tarime, akieleza kuwa kundi hilo limekuwa msaada mkubwa kwake tangu apate changamoto ya ulemavu.

“Ninafurahi sana kwa msaada huu. Natoa wito kwa makundi mengine ya kijamii kuiga mfano huu wa kusaidia wenye uhitaji,” amesema Peter.

Mbali na msaada wa kiti mwendo, kundi la Jambo Tarime limeahidi kutoa kiasi cha shilingi laki tano kama mtaji kwa mke wa Peter ili kuendeleza biashara zake ndogo kwa lengo la kukuza uchumi wa familia yao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!