Latest Posts

KUNDO ATIKISA BARIADI, MADARAJA, BARABARA, UMEME NA AFYA VYANG’AA NDANI YA MIAKA MITANO

Mbunge wa Jimbo la Bariadi na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Andrew Kundo, leo Jumapili Mei 4, 2025, ameibua shamrashamra katika Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

 

Akizungumza mbele ya Mgeni Rasmi wa mkutano huo, Ndugu Leyla Ngozi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mlezi wa chama Mkoa wa Pwani, Mhandisi Kundo ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za miundombinu, nishati, afya na mawasiliano.

 

“Nilimfikishia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu hitaji la wanabariadi, akaridhia na kutoa Shilingi bilioni 2.7 kwa ujenzi wa barabara za lami Dutwa na Nkololo, pamoja na bilioni 6.6 kwa ujenzi wa barabara 123 kwa kiwango cha changarawe,” alisema Kundo.

 

Kwa upande wa miundombinu, Mhandisi Kundo ameeleza kuwa tangu mwaka 1961 hadi 2020 Bariadi ilikuwa na madaraja 38 pekee, lakini ndani ya miaka mitano ya uongozi wake, madaraja 45 mapya yamejengwa, yakiwemo Ngashanda, Kidamleda na Senane, na kufanya idadi kufikia 83.

 

Katika sekta ya nishati, amebainisha kuwa hadi mwaka 2020, vijiji 32 pekee kati ya 84 vilikuwa na umeme, lakini kwa sasa vijiji vyote vimeunganishwa na huduma hiyo huku hatua ya kusambaza umeme vitongojini ikiendelea.

 

Kadhalika, ameeleza kuwa mwaka 2020 Bariadi ilikuwa na minara 55 ya mawasiliano, lakini sasa jumla ya minara 42 zaidi zimejengwa, hivyo kuongeza uwiano wa mawasiliano kwa wananchi.

 

Mafanikio hayo yalihitimishwa kwa taarifa ya ujenzi wa vituo vitatu vya afya vilivyogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 1.5, pamoja na kuwekwa kwa taa za barabarani katika maeneo mengi ya jimbo hilo, yakiwemo Dutwa na Nkololo.

 

Kwa mujibu wa Kundo, maendeleo hayo ni matokeo ya uongozi imara, ushirikiano wa wananchi na dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo ya dhati.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!