Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Leilah Ngozi, ametoa wito kwa wananchi wa Jimbo la Bariadi kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Andrew Kundo, kwa kazi nzuri anayofanya katika kusukuma gurudumu la maendeleo jimboni humo na kitaifa.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo uliofanyika leo Jumapili Mei 04, 2025 , Leilah amwsema Mhandisi Kundo ameonesha uongozi wa mfano katika nafasi zote alizowahi kushika, na kwamba mchango wake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaonekana wazi.
“Ninampongeza Mbunge wa Jimbo la Bariadi na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Andrew Kundo, kwa ubunifu na kazi nzuri alizofanya katika majukumu yake ya unaibu waziri katika wizara mbalimbali alizoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia katika Jimbo la Bariadi amefanya makubwa. Kwenye maendeleo hapahitaji mabadiliko,” alisema Leilah.
Amesisitiza kuwa iwapo Jimbo la Bariadi litagawanywa au kutokea mabadiliko yoyote ya kimuundo, wananchi hawapaswi kusita kuendelea kumwamini na kumchagua Mhandisi Kundo, kwa kuwa tayari ameshathibitisha uwezo wake wa uongozi kwa vitendo.
Amewataka wananchi kufanya uamuzi wa busara kwa kuchambua historia ya utendaji wa viongozi waliopo dhidi ya wale wanaotaka nafasi, akisisitiza kuwa kiongozi anayejali maendeleo huonekana kwa kazi zake, si kwa maneno wala ahadi.
Leilah amemtaja Kundo kuwa ni mzalendo na muumini wa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, na kwamba amekuwa mstari wa mbele katika kuyatangaza mafanikio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la wapiga kura ili kushiriki kikamilifu katika chaguzi zijazo, kama njia ya kumheshimu Rais Samia na kuyaendeleza maendeleo.
Aidha, amewataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaojitokeza na kutumia fedha ili kununua uongozi, akisema kuwa viongozi wa namna hiyo hawana nia ya kweli ya kuwatumikia wananchi bali kurudisha gharama walizotumia.
“Hakuna chama mbadala kama Chama cha Mapinduzi. Chama hiki kitaendelea kuongoza kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu hadi mwisho wa dunia,” alihitimisha Leilah, huku akisisitiza haja ya kudumisha mshikamano, amani na maadili ya kisiasa miongoni mwa Watanzania.