Latest Posts

M23 YAPINGA UINGILIAJI WA SADC KIJESHI DRC, YADAI SULUHISHO LIKO NDANI YA NCHI

Katika barua ya wazi kwa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), muungano wa makundi ya waasi na kisiasa nchini Congo la Alliance Fleuve Congo (AFC) unaojumuisha kundi la M23, umejitokeza kupinga vikali uamuzi wa SADC wa kupeleka vikosi vyake Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika barua hiyo iliyoandikwa saa chache kabla ya mkutano wa pamoja wa SADC na EAC, AFC inasisitiza kuwa mgogoro wa DRC ni wa kisiasa, wa utambulisho na wa ndani, hivyo unahitaji suluhisho la ndani badala ya maingilio ya kijeshi kutoka nje.

Mratibu wa AFC, Corneille Nangaa Yobeluo, ameandika: “Tunachukua hatima ya nchi yetu mikononi mwetu kwa mujibu wa Katiba ya DRC. Hatuwezi kuruhusu vikosi vya nje kusaidia serikali isiyo halali ambayo inakandamiza watu wake na kuhatarisha umoja wa taifa.”

Katika barua hiyo, AFC inabainisha kuwa M23 ni sehemu ya harakati yao, wakisisitiza kuwa mapambano yao si uasi bali ni mapinduzi ya kikatiba dhidi ya kile wanachokiita “utawala wa mabavu wa Félix Tshisekedi.” Wanaeleza kuwa utawala huo umegeuka kuwa tishio kwa wananchi kwa kujihusisha na ukandamizaji wa kisiasa, rushwa, na kuendeleza siasa za kikabila.

AFC inashutumu vikali SADC kwa kutumia mkataba wa ulinzi wa pamoja (SADC Mutual Defence Pact, 2003) kama sababu ya kuingilia mgogoro huo. Wanasema kuwa mkataba huo unasisitiza kutohusisha majeshi ya nje katika masuala ya ndani ya nchi mwanachama isipokuwa tu pale ambapo kuna uvamizi wa nje.

“Jeshi la SADC linajihusisha na vita vya ndani vya DRC kwa kuunga mkono utawala unaowakandamiza wananchi wake. Huu si ulinzi wa amani, bali ni kuchochea vita vya ndani.” Anaonya Nangaa.

Aidha, barua hiyo inamshutumu Rais wa DRC Felix Tshisekedi kwa kugeuza jeshi lake kuwa chombo cha ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa na kwa kushirikiana na vikundi vya wapiganaji wa kigeni kama FDLR, jambo ambalo AFC inadai kuwa ni tishio kwa wananchi wa DRC na ukanda mzima wa Maziwa Makuu.

“Tshisekedi amebadilisha nchi kuwa uwanja wa vita kwa maslahi yake binafsi. Familia yake inadhibiti maeneo yote ya madini nchini, huku akitumia mgogoro huu kama mbinu ya kulinda biashara yao ya rasilimali za taifa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

AFC inahimiza wakuu wa SADC na EAC kufikiria upya uamuzi wao wa kupeleka majeshi na badala yake kuhamasisha suluhisho la kisiasa. Wanataka mazungumzo ya moja kwa moja kati ya harakati yao na serikali ya Kinshasa ili kupata mwafaka wa kudumu. “Suluhisho la mgogoro huu haliko nje ya DRC, lipo ndani ya watu wa Kongo wenyewe,” inasema AFC.

Kwa mujibu wa AFC, ili kurejesha amani nchini, Tshisekedi anatakiwa kuacha kutumia mamluki wa Ulaya kuwaua raia wa Kongo, kuacha kufadhili FDLR, na kusitisha ushawishi wa kijeshi unaolenga kuendeleza siasa za kikabila.

Barua hiyo inahitimisha kwa wito kwa jumuiya za kimataifa, viongozi wa Afrika, na wananchi wa DRC kusimama kidete dhidi ya kile wanachokiita “udikteta wa Kisasa” wa Tshisekedi na kuhakikisha kuwa mustakabali wa taifa hilo unaamuliwa na wananchi wake wenyewe, si kwa mizinga ya mataifa jirani au makubaliano ya kisiasa yanayopuuza uhalisia wa tatizo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!